Macho yote kwenye mkutano wa kilele wa mazingira duniani
22 Aprili 2021Haya yote yanafanyika katika siku ambayo Umoja wa Ulaya na Uingereza zimetangaza dhamira zao kuu kuhusiana na mazingira.
Baada ya kuwa afisini kwa miezi mitatu tu, Rais Biden atawaalika viongozi 40 kwa mkutano wa siku mbili wa kilele kuhusu mazingira na kuonyesha wazi kwamba Marekani imerudi katika mstari wa mbele wa masuala ya tabia nchi wakati ambapo kuna hofu inayozidi kuhusiana na ongezeko la joto duniani.
Rais Xi Jinping kutoa hotuba muhimu kwenye mkutano wa kilele
Makundi ya wanaharakati wa mazingria wanatarajia kwamba Bidenambaye anashinikiza kupitishwa kwa dola trilioni mbili na bunge la nchi hiyo kwa ajili ya marekebisho ya miundo msingi nchini Marekani, ataongeza maradufu malengo ya Marekani ya kupunguza utoaji wa gesi chafu zinazochangia katika mabadiliko ya tabia nchi.
China imethibitisha kwamba Rais Xi Jinping atahudhuria na kutoa hotuba muhimu. Huu utakuwa mkutano wa kwanza wa kilele wa Xi na Biden kama rais wa Marekani katika wakati ambapo kuna mivutano inayoongezeka baina ya nchi hizo mbili kuhusiana na masuala ya haki za binadamu, biashara na ulinzi. Haya yote yanafanyika siku mbili baada ya mjumbe wa Marekani wa mazingira John Kerry kuizuru Shanghai na kuafikiana na China kuhusiana na ushirikiano katika masuala ya mazingira.
"Ukweli ni kwamba hakuna nchi moja inayoweza kufanikisha jambo hili, hata Marekani ikafikia lengo la kusitisha utoaji wa gesi chafu kabisa, au Uingereza au Ulaya. China ambayo inatoa asilimia 30 ya gesi chafu duniani, nchi zengine kama India, Urusi, Indonesia na Japan, kuna nchi nyingi tu ambazo zinachangia changamoto hii. Kati ya nchi zilizoalikwa na Rais Biden, ishirini zinachangia asilimia 81 ya utoaji wa gesi chafu kwa hiyo nchi hizo zinastahili kuongoza njia," alisema Kerry.
Uingereza inalenga kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa asilimia 78
Kivyovyote vile, hakuna suluhisho linaloweza kuafikiwa bila uwepo wa China na Marekani katika meza ya mazungumzo.
Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye amekosolewa na Biden katika masuala kadhaa yakiwemo mzozo wa Ukraine na mkosoaji wake mkubwa Alexei Navalny, amethibitisha pia kwamba atahudhuria akisema nchi yake ambaye ni ya nne katika utoaji wa gesi chafu duniani, lazima ikabiliane na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
Hapo Jumanne, Uingereza ilitangaza inalenga kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa asilimia 78 ifikiapo mwaka 2035. Waziri Mkuu Boris Johnson alitoa tangazo hilo huku Uingereza ikijiandaa kuandaa mkutano mkuu wa mazingira wa Umoja wa Mataifa mjini Glasgow.
Umoja wa Ulaya nao umetangaza unalenga kupunguza gesi chafu kwa asilimia 55 ifikiapo mwaka 2030. Lakini wanaharakati wa mazingira wanatoa wito kwa mataifa duniani kutotoa ahadi tu na badala yake wachukue hatua.