1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machar asaka muafaka na Museveni

22 Julai 2014

Ujumbe wa waasi wa Sudan Kusini unakutana na rais wa Uganda Yoweri Museveni kwa mazungmzo mjini Kampala Jumanne, kumuomba aondowe vikosi vya nchi yake kutoka Sudan Kusini, ambako vilipelekwa kuisaidia serikali ya Juba.

https://p.dw.com/p/1CgSs
Machar und Kiir in Addis Abeba
Picha: Reuters

Museveni alisema mwezi Januari kuwa vikosi vyake vilikuwa vinamsaidia rais Salva Kiir dhidi ya waasi wanaoogozwa na makamu wake wa zamani Riek Machar. Ushiriki wa vikosi vya Uganda katika mgogoro wa Sudan Kusini umekosolewa vikali na waasi

Mataifa jirani na ya magharibi, pia yana wasiwasi kuwa ushiriki huo unazidisha ugumu katika juhudi za kuukomesha mgogoro huo uliyoibuka miezi saba iliyopita, na ambao unatishia kuitumbukiza nchi hiyo katika janga la njaa.

Ukurasa mpya wa mahusiano

Msemaji wa Riek Machar Miyong Kuon, alisema mjini Addis Ababa kuwa ujumbe huo wa waasi unalenga kufungua ukurasa mpya katika uhusiano baina ya waasi hao na Uganda na pia rais Museveni.

Salva Kiir na Riek Machar wakishikana mikono na padri kabla ya kusaini kwa makubaliano ya amani mwezi Mei mjini Addisa Ababa.
Salva Kiir na Riek Machar wakishikana mikono na padri kabla ya kusaini kwa makubaliano ya amani mwezi Mei mjini Addisa Ababa.Picha: Reuters

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Uganda Fred Opolot hakuweza kutoa maelezo zaidi juu ya ajenda za mkutano huo, lakini alisema mazungumzo yatajikita juu ya kuondoa mkwamo katika mchakato wa amani.

Pande hasimu zimefanya mazungumzo kwa miezi kadhaa mjini Addis Ababa tangu mapigano yalipoibuka katikati mwa mwezi Desemba, lakini kumekuwepo na maendeleo kidogo sana.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Januari na Mei yamevunjika. Kiir na Machar pia walikubaliana mwezi Mei kuanza mazungumzo ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, lakini wazo hilo halijafanyiwa kazi tangu wakati huo.

Alipoulizwa iwapo kuondolewa kwa vikosi vya Uganda kutajadiliwa na Museveni, afisa wa waasi alisema jambo hilo ni sehemu ya ujumbe wao, lakini akaongeza kuwa namna, lini na wapi ndiyo mambo yatakayojadiliwa.

Lakini waziri wa nchi wa masuala ya kigeni Okello Oryem, alisema suala hilo siyo la kujadiliwa, akiliambia shirika la habari la reuters kuwa hakuna atakayewamulia lini waondoke Sudan Kusini.

Rais Museveni amekuwa na uhusiano wa karibu na Kiir, kiongozi wa chama tawala cha SPLA, ambacho kiliongoza mapigano ya zaidi ya miongo miwili dhidi ya serikali ya mjini Khartoum kabla ya Sudan Kusini kujipatia uhuru wake mwaka 2011. Nchi hiyo pia ni kituo muhimu cha mauzo ya nje ya Uganda, na biashara kati ya mataifa hayo iliathiriwa sana na kuibuka kwa mapigano.

Rais Museveni na Salva Kiir.
Rais Museveni na Salva Kiir.Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Waasi wanyooshewa kidole cha lawama

Wakati huo huo, Marekani imelaani shambulio la ardhini lililofanywa na waasi dhidi ya wanajeshi wa serikali katika mji wa kaskazini wa Nassir siku ya Jumapili, na imeonya kuwa Washington itawawekea vikwazo wale wote wanaokwamisha juhudi za amani.

Umoja wa Mataifa na ujumbe wake nchini Sudan Kusini UNMISS ulivilaumu vikosi vya Machar kwa ukiukwaji wa makubaliano ya kusiitsha mapigano.

Licha ya waasi hao kudai kuudhibiti kikamilifu mji huo ambao ni makao yao makuu ya zamani, Umoja wa Mataifa ulisema mapigano yalikuwa yanaendelea, huku makabiliano makali zaidi yakiripotiwa jana Jumatatu karibu na kambi ya wanajeshi wa serikali, magharibi mwa mji huo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre,afpe.
Mhariri: Daniel Gakuba