1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machar akutana na Rais Kiir wa Sudan Kusini

10 Mei 2014

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar wanakutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza tokea kuzuka kwa mzozo nchini mwao mwezi Disemba mwaka jana na kusababisha ukiukaji mkubwa haki za binaadamu.

https://p.dw.com/p/1BxKy
Kiongozi wa waasi Riek Machar akiwa mjini Addis Ababa,Ethiopia kwa mazungumzo na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini. (09.05.2014)
Kiongozi wa waasi Riek Machar akiwa mjini Addis Ababa,Ethiopia kwa mazungumzo na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini. (09.05.2014)Picha: Reuters

Mazungumzo hayo yanafanyika Ijumaa (09.05.2014) katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia kufuatia juhudi za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ambap hivi karibuni walifanya ziara nchini Sudan Kusini.

Machar kwanza alikutana na wanasiasa wanne waandamizi ambao serikali iliwatia mbaroni kwa madai ya kula njama ya kufanya mapinduzi kwa niaba yake na ambao wameachiliwa huru wiki mbili zilizopita.

Duru zilizo karibu na mazungumzo hayo zinasema Machar pia alikuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo na Ushirikiano baina ya serikali za Nchi za Mashariki mwa Afrika (IGAD) ambayo ilikuwa msuluhishi katika mazungumzo hayo ya amani.

Matumaini ya amani

Wawakilishi wa Kir na Machar walikuwa wakikutana kwa miezi kadhaa lakini viongozi hao wenyewe hawakuwahi kukutana ana kwa ana tokea kuzuka kwa mzozo huo wa Sudan Kusini.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry akiwa na Rais Slava Kiir wa Sudan Kusini mjini Juba.(02.05.2014)
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry akiwa na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini mjini Juba.(02.05.2014)Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Mmojawapo wa wanasiasa walioachiliwa huru Pagan Amum amesema ana matumaini thabiti ya kufikiwa kwa amani na umoja kwa nchi yao.Amum ambaye ni katibu mkuu wa zamani wa chama tawala cha Sudan Kusini SPLM amesema wanasubiri kwa hamu kukutana na Rais Salva Kiir kumshawishi juu ya haja ya kukomesha vita hivyo.

Pande hizo mbili hivi karibuni zimekubaliana juu ya usitishaji wa mapigano wa mwezi mmoja ili kuwawezesha wakulima kupanda mazao yao, lakini hata hivyo mapigano yamekuwa yakiendelea.

Mashambulizi ya serikali yaendelea

Brigedia Generali Lul Ruai Koang msemaji wa waasi amesema hata kabla ya mkutano huo kuanza tayari wamekuwa wakipokea taarifa kwamba vikosi vya serikali vinavishambulia vikosi vyao katika majimbo matatu.

Msemaji wa waasi Brigedia Generali Lul Ruai Koang (kushoto), na Gatdet Dak(kulia) msemaji wa Machar wakizungumza na waandishi wa habari Addis Ababa . (09.05.2014)
Msemaji wa waasi Brigedia Generali Lul Ruai Koang (kushoto), na Gatdet Dak(kulia) msemaji wa Machar wakizungumza na waandishi wa habari Addis Ababa . (09.05.2014)Picha: Z.ABUBEKER/AFP/Getty Images

Amesema "Rais Salva Kiir hayuko makini katika suala la kutafuta ufumbuzi wa kisiasa kwa mzozo huu.Anaamini katika kuwa na ufumbuzi wa kijeshi na ndio maana vikosi vyake vinafanya mashambulizi kila mahala."

Koang ameongeza kusema ili kuzungumzia amani kunahitajika kuwepo mazingira mazuri ya kufanya hivyo lakini serikali inaendeleza vita.

Mapambano ya kuwania madaraka kati ya Kiir na Machar yaligeuka kuwa umwagaji damu hapo kati kati ya mwezi wa Disemba wakati yalipozuka mapigano kati ya wanajeshi waliokuwemo kwenye makundi tafauti yanayowaunga mkono ya kabila Dinka na la Nuer. Maelfu ya watu wameuwawa katika mzozo huo na wengine zaidi ya milioni moja wamepotezewa makaazi.

Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu la Amnesty International na Umoja wa Mataifa wiki hii wameyashutumu makundi hayo yanayohasimiana kwa kuchochea unyama unaofanyika kwa misingi ya kikabila ambapo baadhi ya vitendo hivyo vinaweza kuhusishwa na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ dpa/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu