1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko yalazimu wageni kuondolewa Libya

Josephat Nyiro Charo1 Agosti 2014

Mataifa zaidi yamechukua hatua kuwaondoa raia wake kutoka Libya huku machafuko yakizidi kuchacha nchini humo kati ya makundi ya waasi yanayohasimiana.

https://p.dw.com/p/1CnLr
Libyen Treibstofftanks Brand Explosion Rakete Zerstörung Feuer Evakuierung
Picha: Reuters

Ugiriki imetuma meli yake ya jeshi la majini kwenda Libya kufanya operesheni ya dharura ya kuwaondoa Wagiriki na wafanyakazi wa ubalozi wake kutoka taifa hilo. Wizara ya mambo ya kigeni ya Ugiriki inatuma meli hiyo kwa kuwa uwanja wa ndege wa Tripoli ni eneo hatari ambalo haliwezi kutumiwa kuwaondoa raia wake, na meli hiyo inaelekea katika taifa jirani la Tunisia. Wafanyakazi wote wa ubalozi wa Ugiriki pamoja na Wagiriki wapatao 80 wanaoishi Libya wamejulishwa wanaweza kupanda meli hiyo kurudi nyumbani.

Mataifa mengine kama vile China yameomba meli hiyo ya Ugiriki iwasaidie raia wake kuondoka Libya. Mamia ya wafanyakazi Wachina tayari wameondolewa kutoka nchini humo, kama Zahi Guohui, ambaye alikuwa akifanya kazi mjini Tripoli. "Tunafanya kazi na kampuni ya mawasiliano kama simu, lakini sasa kwa sababu ya mapigano Libya ina tatizo kubwa na kwa hiyo lazima turejee China. Naipenda Libya na Walibya na ningependa kurudi. Naomba mapigano yote yakome."

Umoja wa Ulaya umewaondoa kwa muda wafanyakazi wake wa kimataifa kutoka Tripoli. Msemaji wa umoja huo, Michael Mann, amesema Umoja wa Ulaya uko tayari kuwarejesha wafanyakazi wake mjini humo mara tu hali itakaporuhusu. Bwana Mann amesema kazi za kiofisi zitaendeshwa na wafanyakazi raia wa Libya.

Libyen Flughafen Tripolis Mitiga
Mtafuruku katika uwanja wa ndege wa TripoliPicha: Reuters

Wafaransa 40, akiwemo balozi wa Ufaransa nchini Libya, pamoja na Waingereza saba wamewasili katika bandari ya Toulon mapema leo wakitokea Libya. Ufaransa iliwataka raia wake waondoke Jumatatu iliyopita.

Wizara ya afya ya Libya inasema watu 179 wameuwawa kwenye mapigano mjini Tripoli na mji wa mashariki wa Benghazi katika kipindi cha wiki moja tu.

Mfumo wa afya mashakani

Wakati huo huo Libya imeonya kuhusu kuporomoka kabisa kwa mfumo wake wa afya huku machafuko yanayoendelea kulikumba taifa hilo yakitishia kuwafukuza wataalamu wa afya kutoka Ufilipino na India ambao hospitali za Libya zinawategemea sana. Wafanyakazi 3,000 wa afya kutoka Ufilipo, ambao ni asilimia 60 ya wafanyakazi wote wa afya wa Libya, huenda wakaondoka nchini humo, pamoja na wafanyakazi kutoka India ambao kwa jumla ni asilimia 20 ya wafanyakazi wa afya nchini Libya.

Jumatano iliyopita serikali ya Ufilipino mjini Manila tayari iliwahimiza raia wake waondoke Libya kufuatia kutekwa nyara mfanyakazi mmoja Mfilipino ambaye baadaye alipatikana amekatwa kichwa.

Tunisia yatoa onyo

Huku haya yakiarifiwa maelfu ya Walibya wamevuka mpaka kuingia nchini Tunisia jana kutokana na mapigano yanayoendelea nchini mwao. Shirika la habari la serikali ya Tunisia limeripoti kwamba maelfu ya Walibya wamekimbia kutumia usifiri wa magari na kuvuka mpaka katika kipindi cha saa 12 zilizopita.

Libyische Flüchtlinge in Tunesien 2011
Wakimbizi wa Libya nchini TunisiaPicha: Joel Saget/AFP/Getty Images

Waziri wa mambo ya kigeni wa Tunisia, Mongi Hamdi, alisema, "Nawakaribisha ndugu zetu Walibya walio nchini Tunisia. Lakini kwa kuzingatia hali ya usalama inayoendeela kuzorota, na kama itazidi kuwa mbaya, kuna uwezekano tutachukua hatua kuhakikisha usalama na uthabiti wa Tunisia."

Tunisia imetangaza hali ya tahadhari katika mipaka yake huku ikionya huenda ikakabiliwa na kibarua kigumu katika kulishughulikia wimbi kubwa la wakimbizi wanaoikimbia Libya. Imesaema huenda ikalazimika kuufunga mpaka wake kukiwa na haja ya kufanya hivyo.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef