Machafuko ya Sudan yaongeza hofu ya vita
25 Aprili 2012Lakini wakati hayo yakiendelea, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir hii leo anaanza ziara ya kiserikali nchini China, ambako atakutana na mwenyeji wake Hu Jintao. Sudan na Sudan Kusini zimekuwa zikipigana katika miezi ya hivi karibuni katika eeno lao mpaka wao lililo na utajiri wa mafuta, hali iliyoibua hofu kutoka wka jamii ya kimataifa kuhusu uwezekano wa kuzuka vita.
Wito wa Ban kutaka utulivu umejiri baada ya rais wa Sudan Omar al-Bashir kufuta uwezekano wowote wa kufanya mazungumzo na hasimu wake wa Kusini Salva Kiir, ambaye yuko mjini Beijing, kutafuta uungaji mkono kutoka wka China ambaye ni mshirika wa tangu jadi wa Sudan.
Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Eduardo del Buey amesema Ban amekariri kuwa hakuwezi kuwa na suluhu ya kijeshi katika mizozo baina ya Sudan na Sudan Kusini. Amemtaka rais Bashir na rais Kiir kuwacha kujiingiza katika vita na badala yake kurejea katika meza ya mazungumzo haraka iwezekenavyo.
Sudan Kusini ilisema Jumapili kuwa imeviondoa vikosi vyake vyote kutoka jimbo linalogombaniwa la Heglig, lakini mashambulizi ya angani yalifanywa jana Jumatatu Bentiu, ambao ni mji mkuu wa jimbo la upande wa Kusini la Unity.
Kiir yuko mjini Beijing
Salva Kiir ambaye yuko ziarani China anatarajiwa kukutana na mwenzake wa China Hu Jintao baadaye leo katika mazungumzo ambayo huenda yakaulenga mzozo huo kati ya Sudan Kusini na Sudan. China imekuwa rafiki mkubwa wa Sudan na pia mshirika mkuu wa kiuchumi wa Sudan, ambapo imeisaidia kuwa muuzaji mkubwa wa mafuta.
Lakini kujitenga kwa Upande wa Kusini kutoka Kaskazini mwezi Julai mwaka wa 2011, pamoja na machafuko ya hivi karibuni, kumeilazimu China kutokuwa na msimamo wa wazi katika kujaribu kuendelea kuiunga mkono serikali ya Khartoum, lakini wakati huo huo isiitenge serikali ya Juba. Suda Kusini ambalo ni taifa jipya ulimwenguni, ina utajiri mkubwa wa mafuta. China ilitoa wito wa kusitishwa mapigano ya mipakani ambapo Sudan Kusini ilitwaa udhibiti wa eneo muhimu la mafuta Heglig mnamo tarehe 10 Aprili kwa siku 10.
Akiwa mjini beijing, Kiir anatarajiwa kuwasilisha hoja zake kwa mamlaka ya China, lakini wachambuzi wa siasa wanasema China haionekani kuegemea upande wowote katika suala hilo, na badala yake itaendelea kushinikiza kuwepo mazungumzo.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Hamidou Oummilkheir