1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko Sahel yachangia njaa kwa mamilioni ya watu

13 Desemba 2021

Kufuatia athari za mvua zisizotabirika, pamoja na mshambulizi ya wanamgambo vimesababisha takriban watu milioni 5.5 katika mataifa matatu ya Burkina Faso, Mali na Niger wanakabiliwa na uhaba wa chakula. 

https://p.dw.com/p/44BzX
Burkina Faso |  Siedlung für Binnenflüchtlinge
Picha: Giles Clarke/UNOCHA

Umoja wa Mataifa unakisia kwamba idadi hiyo itaongezeka hadi kufikia watu milioni 8.2 ifikapo mwezi Agosti wakati ambapo kwa kawaida uhaba mkubwa wa chakula hushuhudiwa kabla ya kipindi cha mavuno kuanza.

Sakinatou Amadou mwenye umri wa miezi tisa anaendelea kupona baada ya kuathiriwa na utapiamlo. Mama yake Sakinatou aliaga dunia hivyo kumuacha Sakinatou akilelewa na bibi yake katika kituo kidogo cha kibiashara Dori, karibu na mpaka wa nchi yao Burkina Faso na Niger. Bibi ambaye pia familia yake ya watu 14 imekuwa ikihangaika kujikimu kimaisha tangu walipokimbia kutoka kijiji chao mwaka 2019.

Soma: Burkina Faso ipo katikati ya vita na maandamano

Wao ni kati ya watu milioni 2 nchini Burkina Faso, Mali na Niger waliolazimika kuyakimbia makaazi yao kufuatia wimbi la mashambulizi yanayofanywa vijijini na makundi yenye itikadi kali za dini ya Kiislamu.

Kumekuwa na ongezeko la watu wanaoyakimbia makaazi yao kufuatia machafuko katika nchi za MAli, Burkina Faso na Niger
Kumekuwa na ongezeko la watu wanaoyakimbia makaazi yao kufuatia machafuko katika nchi za MAli, Burkina Faso na NigerPicha: imago images/Joerg Boethling

Huku mazao mashambani yakiwa hafifu kutokana na athari za mvua zisizotabirika, takriban watu milioni 5.5 katika nchi hizo zilizoko katika kingo za jangwa la Sahara, wananyemelewa na uhaba wa chakula. 

Daktari Alphonse Gnoumou ambaye anasimamia zahanati moja katika kijiji cha Dori na ambaye alimsaidia Sakinatou kurejesha uzito baada ya kuugua utapiamlo, amesema kufuatia mvua zisizotabirika, watu wamepoteza mifugo, mimea na hata mazao.

Soma: Guterres alaani mauaji ya watu 160 nchini Burkina Faso

Kadidiatou Ba ambaye huuza mboga na bidhaa nyingine zilizokaushwa katika kioski ya kando ya barabara, amesema soko la mifugo ambalo lilikuwa na shughuli nyingi katika mji huo tayari limefungwa kufuatia machafuko. Ameongeza kuwa imekuwa hatari siku hizi kusafirisha bidhaa au vyakula katika eneo hilo. Isitoshe bei ya bidhaa zimepanda na kuwa ghali.

”Kila kitu kimepanda bei. Tulikuwa tukilipa Faranga 40,000 (sawa na dola 68) kwa kila gunia la maharage, lakini sasa tunalipa faranga 75,000,” amesema hayo huku akisubiri wateja.

Mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa makundi ya wanamgambo wanaoshikilia itikadi kali za dini ya Kiislamu ni kati ya mambo yanayodaiwa kuchangia mamilioni ya watu kukumbwa na njaa.
Mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa makundi ya wanamgambo wanaoshikilia itikadi kali za dini ya Kiislamu ni kati ya mambo yanayodaiwa kuchangia mamilioni ya watu kukumbwa na njaa.Picha: Sophie Garcia/AP/picture alliance

Jambo jingine ni kwamba idadi ya watu katika mji wa Dori imeongezeka zaidi ya mara tatu katika kipindi cha miaka miwili hadi kufikia watu 71, 000. Na ongezeko la wakimbizi linatishia kulemea huduma hafifu zilizoko katika eneo hilo.

Hali katika shule iliyoko karibu nayo si ya kuridhisha. Wanafunzi wanne hung'ang'ana kuketi kwenye dawati moja ili kupata sahani ya wali kwa maharage, ndipo angalau mkono uelekee kinywani japo mara moja kwa siku.

Bokum Abdalaye, mwalimu mkuu wa shule hiyo amesema, watoto hao walitatizika mno akili. "Walipokuja hapa na wazazi wao, tuliwaona wakiwa wamejawa huzuni masikitiko.” Huku wanafunzi hao wakicheza, karibu naye Abdalaye anasema hatua ya kuwapa watoto hao mlo wa mchana na wanakula pamoja, imewasaidia kuishi kwa kutulia.

(RTRE)