Machafuko Madagaskar
27 Januari 2009Rais Marc Ravalomanana wa Madagaskar, ameitisha leo mazungumzo na mpinzani wake ,meya wa mji mkuu Antananarivo, Andry Rajoelina. Rajoelina kwa upande wake, amesimamisha maandamano yote dhidi ya serikali kwa leo baada ya mfuasi wa Upinzani kupigwa risasi na mwanajeshi hapo jana.Isitoshe,amewataka wafuasi wake kubakia nyumbani.
Machafuko yanayozidi kisiwani Madagaskar yalimlazimisha Rais Ravalomanana aliekuja madarakani kufuatia uchaguzi wa utata wa 2001,akatize ziara yake ya Afrika Kusini juu ya mzozo wa zimbabwe na kurejea haraka nyumbani hapo Jumapili.Kiongozi wa upinzani,meya wa Antananarivo,Andry Rajoelina alieongoza jana maandamano makali dhidi ya serikali ya Ravalomanana alioiita ni ya "kidikteta", amesema kwa leo hakuna mazungumzo.
kiongozi huyu wa Upimnzani anadai kwanza mwanajeshi aliemuua mmoja wa wafuasi wake ahukumiwe.Mfuasi huyo anaripotiwa amepigwa risasi na mwanajeshi wa serikali hapo jana m bele ya Kituo cha TV cha MBS ambacho kama Kituo Kikuu cha Radio ilizingirwa na umati uliokasirika.
"Nawataka wabuki kutulia.Inatubidi kuweka kando majivuno yetu na matakwa yetu na yatubi tuzungumze." alisema rais Ravalomanana kupitia kituo cha Radio ya kibinafsi "ANTSIVA".
Rais aliongeza kwamba ameshaanza mawasiliano fulani na mpinzani wake.
Leo hakukuwa na maandamano mjini Antananarivo,mji mkuu wa Bukini -jina jengine la Madagascar.
hata hivyo, kulikuwepo vikundi vidogo-vidogo mjini Antananarivo hii leo asubuhi na weengineo wakajikusanya katika bustani la jiji hilo ambako meya Rajoelina alifanya mkutano mkubwa wa hadhara hapo jumamosi.
Kwa muujibu wa usalama Lucien Emmanuel Raharijaona alivyowaambia maripota si chini ya watu 2 waliuwawa katika machafuko ya jana.Hakueleza zaidi. Aliwataka wananchi wote wa Madagascar kuonesha dhamana zao na kuvisaidia vikosi vya usalama kuhakikisha wabuki wanarejea shughuli zao za kawaida haraka iwezekanavyo.
Nae makamo wa meya Rajoelina aliarifu kuwa mtu mmoja alieandamana alikandikwa risasi kichwani na wanajeshi mbele ya kituo cha kibinafsi cha TV kinachomilikiwa na rais -MBS.
Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika , Jean Ping amesema na niknamnukulu,
"tunaiangalia hali ya mambo kwa makini kisiwani madagaskar ambayo inazidi kuwa tatizo."
Ping aliongeza kusema kwamba Jumuiya ya SADC pia inaukodolea macho msukosuko kisiwani Madagaskar.
Meya wa Antananarivo Rajoelina, amekuwa akipalilia upinzani dhidi ya serikali tangu mwezi uliopita pale ilipokifunga kituo chake cha TV VIVA kwa kuwa tu kilitangaza mahojiano na Rais wa zamani Didier Ratsiraka .
Ratsiraka aliyeitawala Madagaskar kwa kipindi cha miaka 25 hivi sasa anaishi uhamishoni nchini Ufaransa baada ya mvutano mkubwa wa kisiasa na rais wa sasa Ravalomanana.