1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko Iraq yarindima

21 Oktoba 2013

Nchini Iraq vikosi vya usalama vimetangaza amri ya kutotoka nje katika mji wa Fallujah kufuatia mapigano yaliyozuka katika mji huo.Watu wenye silaha wamepambana na vikosi vya usalama.

https://p.dw.com/p/1A3Mm
Waziri mkuu wa Iraq Nuri al-Maliki
Waziri mkuu wa Iraq Nuri al-MalikiPicha: picture-alliance/dpa/dpaweb

Moto unawaka nchini Iraq katika mji wa Al Fallujah ambako amri ya kutotoka nje imetangazwa .Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha kujitegemea cha Alsumaria amri hiyo imetangazwa huku maafisa wawili wa polisi wakiwa wameuwawa mapema hii leo pale washambuliaji wakujitowa muhanga walipojiripuwa katika makao makuu ya polisi ambayo baadae yalishambuliwa kwa mapambano ya risasi na mizinga.

Baadae washambuliaji hao walikimbilia katika jengo la kampuni moja ya umeme ambako waliwateka nyara wafanyakazi wote wa kampuni hiyo waliokuweko ndani.Inaarifiwa polisi imefanikiwa kuwauwa wateka nyara wawili na kuwakombowa watu wawili waliokuwa miongoni mwa wanaoshikiliwa mateka.Hilo ni shambulio la pili ndani ya siku mbili kwa mujibu wa maafisa pamoja na madaktari waliozungumza na vyombo vya habari.

Iraq inakabiliwa na ghasia mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 2008 wakati nchi hiyo ilipoanza kujikwamuwa kutokana na mgogoro wa kimadhehebu uliosababisha unyama mkubwa na sasa maafisa katika taifa hilo wameshindwa hadi wakati huu kukabiliana na ongezeko la machafuko.Ghasia zilianza na tukio la mshambuliaji wa kujitowa muhanga kujiripuwa nje ya jengo la makao makuu ya polisi katika Fallujah mji ulioko magharibi ya Iraq wakati mshambuliaji wa pili akiendesha hujuma katika jengo la karibu na hapo la kampuni ya umeme.

Maandamano ya kuipinga serikali Februari 2013 katika mji wa Fallujah
Maandamano ya kuipinga serikali Februari 2013 katika mji wa FallujahPicha: Reuters

Baadae wanamgambo hao waliyashambulia makao makuu ya polisi kutokea pande tatu kwa risasi,mizinga,na maguruneti na kisha kuingia katika jengo hilo la kampuni ya umeme na kujibanza katika kona mbali mbali walikofyetuwa risasi za shabaha.Mashambulio hayo yamechukuwa roho za maafisa wawili akiwemo meja pamoja na kuwajeruhi wengine wanne.Hata hivyo msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Brigedia Generali Saad Maan amesema vikosi vya usalama vimefanikiwa kuwauwa waripuaji watano wakujitowa muhanga katika mji huo.

Ni mashambulio ambayo yametokea siku moja baada ya mashambulio ya kuratibiwa kufanywa dhidi ya majengo ya serikali katika mji wa Rawa mji ambao uko kaskazini ya Fallujah katika mkowa wa Anbar.Watu wanane wamepoteza maisha yao katika hujuma hizo.Sura hiyo ya machafuko inajitokeza katika wakati ambapo mjumbe wa Kimataifa kuhusu Syria Lakhdar Brahimi yuko Baghdad kwajili ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa nchi hiyo ya Syria.

Fallujah mji unaokabiliwa mara kwa mara na machafuko Iraq
Fallujah mji unaokabiliwa mara kwa mara na machafuko IraqPicha: Reuters

Brahimi ameingia moja kwamoja katika mazungumzo na waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki ingawa hadi sasa hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa kufuatia kikao chao.Brahimi anatokea Cairo Misri ambako jana Jumapili alikutana na mkuu wa jumuiya ya nchi za Kiarabu Nabil al Arabi na akitarajiwa kuelekea pia Iran Qatar na Uturuki pamoja na uwezekano wa kwenda Syria kwenyewe.Iraq hadi sasa inajizuia kuchukuwa msimamo wa wazi juu ya vita vya Syria kati ya utawala wa Assad na waasi wanaotaka kuupinduwa lakini mgogoro huo umevuka mpaka mara kadhaa na kuingia hadi nchi hiyo.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri AbdulRahman Mohammed