1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko Ecuador

Kabogo Grace Patricia1 Oktoba 2010

Mataifa ya Amerika yameelezea nia ya kumsaidia Rais Rafael Correa wa Ecuador baada ya polisi na wanajeshi kuasi.

https://p.dw.com/p/PRiU
Mapolisi na wanajeshi wakiwa katika maandamano nchini Ecuador.Picha: AP

Mataifa mbalimbali ya Amerika, zikiwemo Brazil na Marekani zimeelezea nia yao ya kumsaidia Rais Rafael Correa wa Ecuador kutokana na uasi uliofanywa na polisi na baadhi ya wanajeshi wenye vyeo katika mji wa Quito.

Kiongozi huyo wa mrengo wa shoto alikimbilia kuomba hifadhi hospitali baada ya kuzidiwa na mabomu ya kutoa machozi wakati wa mapambano ya kutupiana maneno na polisi wanaopinga kile wanachosema ni kupunguzwa kwa malipo.

Kundi la wanajeshi 150 pia waliufunga uwanja wa ndege wa Quito baada ya kudhibiti njia ya kupita ndege. Serikali ya Correa imetangaza hali ya hatari. Pia kuna hali ya machafuko katika mji mwingine mkubwa wa Guayaquil.

Mkuu wa majeshi, Ernesto Gonzalez amesema wanajeshi wanaendelea kuwa watiifu kwa Rais Correa. Kiongozi huyo aliyepata mafunzo yake ya uchumi nchini Marekani alichaguliwa tena mwaka uliopita kwa msimamo mgumu kuelekea sera zisizozuilika za soko huru na kukataa kulipa madeni ya nje. Ecuador imekuwa na marais wanane katika kipindi cha miaka 13.