1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maas atoa wito wa mageuzi ya Baraza la Usalama

29 Septemba 2018

Waziri wa mambo ya Nchi za Kigeni wa Ujerumani Heiko Maas amelitaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hatimaye kuanzisha mazungumzo muhimu kuhusu mageuzi katika Baraza la Usalama la umoja huo.

https://p.dw.com/p/35gcG
USA l Außenminister Maas - UN-Rede in New York
Picha: Reuters/E. Munoz

Maas amesema Baraza hilo halijabdilika tangu lilipoasisiwa mwaka wa 1945, licha ya kuongezeka mara tatu kwa idadi ya watu duniani tangu wakati huo, na kuongezeka mara nne idadi ya nchi wanachama katika kipindi hicho.

Ujerumani kwa muda mrefu imekuwa ikishinikiza megeuzi ya Umoja wa Mataifa na lengo kuu la kutaka kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama. China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani ni wanachama wa kudumu wakiwa na kura za turufu kuhusu maamuzi ya Baraza hilo.

Ujerumani imechaguliwa kuwa mmoja wa wanachama 10 wasio wa kudumu kwa muhula mmoja wa miaka miwili kuanzia Januari 2019.

Maas amesema wakati wa hotuba yake kwa baraza hilo kuwa ni aibu kwamba shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia Wakimbizi UNHCR linapungukiwa na fedha za kuwasaidia mamilioni ya Wasyria ambao wamekimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Ameyataka mataifa mengine tajiri kutoa mchango.

Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani amesema nchi yake itatoa euro milioni 116 za ziada kusaidia kukabiliana na idadi kubwa ya Wasyria wanaomiminika katika nchi jirani za Kiarabu.

USA, New York: Tag Drei:UN Wahl 2019-2020
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/dpa/Y. Jansens

Maas pia ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa mzozo kuhusu diplomasia ya kimataifa unaweza kutatuliwa, akitoa mfano wa Ujerumani kufuatia kuangishwa kwa Unazi. Alisema ujasiri wa majirani wa Ujerumani barani Ulaya katika kutafuta maridhiano na msaada wa Marekani umeliweka bara hilo kwenye mkondo wa uhuru, usalama na ustawii baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Katika hotuba zao, Urusi na China zilijiweka katika nafasi ya kuwa watetezi wa msingi wa ushirikiano wa mataifa ya ulimwengu ambayo yanatimiza ahadi wakati Marekani ikijitenga.

Waziri wa mambo ya kigeni wa China Wang Yi alikanusha kuwa nchi yake inajaribu kushindana na Marekani kama taifa kubwa duniani, lakini hotuba yake ilikuwa tofauti kabisa na ujumbe wa Trump wa "Marekani Kwanza”. Ilikuja wakati kukiwa na ongezeko la mvutano kati ya Marekani na China, ambayo Trump aliituhumu wiki hii kwa kuingilia uchaguzi wa mwaka huu wa katikati ya muhula nchini Marekani. China inakanusha madai hayo.

Katika wiki ambayo Marekani iliongeza viwango vya ushuru kwa bidhaa za China nayo China ikajibu kwa kufanya hivyo hivyo, Wang amesisitiza kuwa nchi yake haitasalitiwa au kusalimu amri na akaonya kuwa sera za ulinzi wa masoko inamuathiri tu anayeitekeleza na kuwa hatua za kuzingatia taifa binafsi itasababisha uharibifu kwa wote. Ameongeza kuwa mahusiano kati ya taifa moja na jingine yanapaswa kuzingatia uaminifu na sio kuvunja tu ahadi wakati wowote unapotaka

Urusi pia inakabiliwa na tuhuma za kuingilia uchaguzi wa Marekani, ambazo Wazuri wa Mambo ya Kigeni Sergey Lavrov alisema sio za msingi. Lavrov aliitumia hotuba yake kuzishambulia sera za Marekani nchini Iran, Syria na kwingineko na akayatetea vikali mashirika ya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iraq Ibrahim al-Jaafari aliipongeza jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kwa msaada wake katika vita dhidi ya kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu – IS.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Gakuba, Daniel