1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano zaidi yafanyika Marekani

26 Novemba 2014

Maandamano yalisambaa kote nchini Marekani kwa siku ya pili wakati zaidi ya askari 2,000 wakipelekwa katika eneo la St. Louis ili kuzuia visa vya vurugu na uporaji mali

https://p.dw.com/p/1Dtot
Proteste gegen den Ferguson Urteil 25.11.2014
Picha: Reuters/J. Young

Hii ni baada ya jopo la wazee wa baraza la mahakama kukataa kumfungulia mashtaka polisi mweupe aliyempiga risasi na kumuua kijana mweusi ambaye hakuwa na silaha. Askari waliwatawanya waandamanaji kutoka barabara za kitongoji cha Ferguson baada ya usiku wa pili wa maandamano kufuatia uamuzi wa jopo la wazee wa baraza la mahakama kutomfungulia mashtaka polisi Darren Wilson aliyemuua kwa risasi kijana Michael Brown.

Maandamano ya leo yalikuwa tulivu kuliko ya jana japokuwa wazima moto waliingilia kati baada ya gari la polisi kuchomwa moto nayo magenge ya wahalifu yakaharibu maduka kadhaa. Zaidi ya watu 40 walikamatwa, katika maandamano ya leo.

Rais Barack Obama amelaani vitendo vya uharibifu na uporaji mali ambavyo alisema ni vya kihalifu na waliohusika wanastahili kuchukuliwa hatua za kisheria. Alitoa wito wa kuwepo mazungumzo kuhusiana na suala la utekelezwaji wa sheria nchini Marekani. Obama alisema "Kwa wale wanaodhani kilichotokea Ferguson ni sababu ya kuzusha machafuko, sina huruma yoyote kuhusu hilo. Sina huruma kabisa kwa kuharibu jamii zenu wenyewe. Lakini kwa watu wengi ambao wanahisi uchungu, kwa sababu wanaona kuwa huenda baadhi ya jamii hazitendewi haki au baadhi ya watu hawaonekani kuwa sawa na wengine, hilo naelewa. Na nataka kufanya kazi nanyi na nataka kusonga mbele nanyi".

Proteste gegen den Ferguson Urteil 25.11.2014
Polisi zaidi wamewekwa mjini Ferguson ili kuzuia uharibifu na uporaji maliPicha: Reuters/L. Jackson

Mwanasheria mkuu Eric Holder aliahidi kuwa uchunguzi wa serikali kuhusiana na kisa cha mauaji ya Brown utafanywa kwa wakati unaofaa. "Ipo haja ya kuwaleta watu pamoja. Huu ni wakati mgumu. Kwa watu wa Ferguson na ni wakati mgumu kwa watu wa nchi hii. Nadhani ni fursa ya sisi kutafuta vitu vinavyotuleta pamoja kama taifa. Kuwa wakweli miongoni mwetu kuhusu mambo hayo yanayoendelea kutugawanya na kutafuta mbinu za kuufanya muungano huu kuwa bora zaidi"

Wilson, ambaye angekabiliwa na mashtaka ya mauaji au kuua bila kukusudia, ameiambia televisheni ya Marekani ya ABC News kuwa hakuna chochote angefanya tofauti wakati wa makabiliano yake na Brown ambacho kingezuia kifo cha kijana huyo. Alisema hajutii kitendo hicho kwa sababu anajua alifanya jambo la kweli kulingana na mazingira aliyokuwamo, akiongeza kwamba angefanya hivyo hivyo hata kama Brown angekuwa mweupe.

Nakala zilizotolewa na waendesha mashtaka zilisema kuwa Wilson ambaye alipewa likizo ya lazima baada ya tukio hilo, aliliambia jopo la wazee wa baraza la mahakama kuwa Brown alijaribu kumpokonya bastola yake, na kuwa ofisa huyo akahisi maisha yake yalikuwa hatarini wakati akifyatua risasi.

Maandamano yalisambaa kutoka Los Angeles hadi Washington. Mjini New York, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuudhibiti umati baada ya waandamanaji kujaribu kuzifunga barabara. Katika majimbo ya Oklahoma, California na Atlanta, waandamanaji walizuia magari, wakati pia mjini Boston kukishuhudiwa maandamano.

Mwandishi: Bruce Amani/reuters
Mhariri:Josephat Charo