1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yavunjwa Viongozi wa upinzani mbaroni Zimbabwe

Mohamed Dahman12 Machi 2007

Polisi wa kutuliza ghasia nchini Zimbabwe wamemtia mbaroni kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo na kumuuwa kwa kumpiga risasi mtu mmoja wakati walipovunja mkutano wa hadhara uliopangwa kuiombea Zimbabwe na kumpinga Rais Robert Mugabe.

https://p.dw.com/p/CHIP
Serikali ya Rais Robert Mugabe pichani yashutumiwa kwa kushambulia raia wake.
Serikali ya Rais Robert Mugabe pichani yashutumiwa kwa kushambulia raia wake.Picha: dpa

Mashahidi wamesema polisi walipambana na wafuasi wa upinzani waliokuwa wakirusha mawe katika kitongoji kimoja cha mji mkuu wa Harare cha Highfiled ambapo waandalizi wa maandamano hayo walijaribu kuandaa mkutano wa hadhara kuzungumzia mgogoro wa kisiasa na kiuchumi unaozidi kukua nchini Zimbabwe.

Polisi ilimkamata kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC Morgan Tsvangirai na viongozi wengine wa upinzani baada ya kuuzuwiya msafara wao wa magari kwenda kwenye eneo la mkutano.

Chama hicho cha upinzani kimesema Tsavangirai na viongozi wengine wameshambuliwa vibaya na kwamba mfuasi mmoja wa MDC ameuwawa kwa kupigwa risasi.

Mvutano wa kisiasa umekuwa ukizidi kupamba moto nchini Zimbabwe wakati nchi hiyo ikizidi kuzama kwenye dimbwi la matatizo makubwa kabisa ya kiuchumi kuwahi kushuhudiwa na nchi hiyo kwa miongo kadhaa ambapo gharama za maisha zimepanda kupindukia asilimia 1,700, ukosefu wa ajira unakaribia asilimia 80 na kuna uhaba wa chakula, mafuta na fedha za kigeni.

Mugabe mwenye umri wa miaka 83 ambaye amekuwa madarakani tokea uhuru wa nchi hiyo hapo mwaka 1980 anakidharau chama cha MDC kuwa ni kibaraka wa utawala wa ukoloni wa Uingereza.

Mjini Washington Marekani msemaji wa Wizara ya mambo ya nchi za nje ya nchi hiyo Sean McCormak amesema katika taarifa kwamba serikali ya Marekani inaalani hatua za ukatili zisizozihitajika za serikali ya Zimbabwe katika kuwashambulia raia wake waliokusanyika kwa amani kutumia haki zao za halali za kidemokrasia.

McCormack amesema wanamwajibisha Rais Robert Mugabe na serikali yake kwa vitendo vyao hivyo na kwa usalama wa uzima wa wale walioko mbaroni.

Msemaji wa polisi ya Zimbabwe Wayne Bvudzijena amesema kwamba polisi wakiwa kwenye doria wamemuuwa mtu mmoja baada ya polisi hao kushambuliwa na wahuni wa chama cha MDC katika eneo la maduka na kwamba polisi watatu wamejeruhiwa vibaya.

Amesema kundi jengine la wahuni hao limetia moto gari la kijeshi na kushambulia polisi waliokuwa katika doria wakati wakiwatumia watoto kama ngao.

Na kwa mujibu wa Katibu mwenezi wa chama cha MDC Elias Mudzuri Morgan Tsvangirai,wasaidizi wake,viongozi wa kiraia na maafisa kadhaa waandamizi wa MDC wamekamatwa na kuwekwa mahabusu bila ya kufunguliwa mashtaka na pia wamepigwa.

Mwanchama mwandamizi wa chama cha MDC Eddie Cross anasema wasi wasi wao mkubwa ni kwamba Morgan amepigwa hakuruhusiwa kuonana na mawakili wake na wakati wakili wake alipojaribu kuonana naye alipata mkon’goto wa polisi.

Cross anasema wanakabiliana na taifa la kihuni.

Katika taarifa Muungano wa kuikoa Zimbabwe umesema mawakili wamekuwa wakinyimwa nafasi ya kukutana nao mahabusu na polisi imewakamata wanaharakati watano wanafunzi katika warsha moja mjini Harare.

Taarifa hiyo imesema polisi wa kutuliza ghasia imelazimisha kufungwa kwa maduka,vilabu vya pombe na makanisa pamoja na kupiga watu kwenye kumbi za pombe.

Kundi hilo linasema kitongoji cha Highfiled kimegeuka kuwa medani ya vita.