Maandamano yarindima Khartoum Sudan
6 Aprili 2022Nchini Sudan vikosi vya usalama vimetumia gesi ya kutowa machozi vikiyalenga maandamano makubwa ya kupinga mapinduzi yaliyofanywa na jeshi nchini humo.
Maandamano ya leo yanakuja katika wakati ambapo nchi hiyo inaadhimisha kumbukumbu ya harakati zilizofanyika mwaka 1985 zilizomuondowa madarakani rais wa wakati huo Jaafar Nimeiri aliyeiongoza Sudan kwa mkono wa chuma.
Katika mji mkuu Khartoum vikosi vya usalama vimetumia gesi ya kutowa machozi dhidi ya umma wa mamia ya waandamanaji. Mashahidi wamesema vikosi vya usalama pia vilivamia hospitali ya al-Jawda na kurusha makopo ya gesi ya kutowa machozi ndani ya hopistali hiyo na kuwatisha wagonjwa pamoja na watoa huduma za afya. Tukio hilo lilisababisha baadhi ya watu kukosa hewa kwenye hospitali hiyo kwa mujibu wa kamati kuu huru ya madaktari wa Sudan.
Maandamano yamefanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwa ni hatua inayoaadhimisha msururu wa matukio ya kihistoria yaliyowaondoa madarakani viongozi wakiimla nchini humo, ikiwemo rais Omar El Bashir aliyeondolewa miaka mitatu iliyopita akiwa ndie kiongozi wa karibuni kabisa kuondolewa kwa nguvu madarakani.
Lakini pia ni maandamano ambayo yanakuja katika wakati ambapo Sudan inakabiliwa na mkwamo wa kisiasa na hali ngumu ya kiuchumi baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoshuhudiwa Oktoba 25 yakiongozwa na mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan.
Maandamano hayo pia yanaadhimisha miaka mitatu tangu zilipoanza harakati za kupiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum ambapo umma wa wasudan waliandamana kwa miezi wakidai utawala wa Omar el Bashir uondoke madarakani, na hatimae Aprili 11 mwaka 2019 Bashir alipinduliwa na majenerali wakuu wa jeshi la nchi hiyo. Ingawa waandamanaji waliendelea kupiga kambi na kudai utawala wa kiraia uwekwe madarakani lakini Juni mwaka huo huo 2019 maandamano hayo yaliyovunjwa kwa nguvu za kijeshi na kwa mujibu wa madaktari kiasi watu 128 waliuwawa katika vurugu hizo zilizoendelea kwa siku nne.
Baadae lakini vuguvugu la kiraia na viongozi wa kijeshi walikubaliana na kuunda serikali ya mpito kuelekea utawala kamili wa kiraia lakini mnamo mwezi Oktoba viongozi wa kijeshi wakafanya tena mapinduzi ya kuwaondowa raia serikalini na kuvuruga mipango yote ya nchi hiyo kuelekea utawala kamili wa kiraia. Na tangu wakati huo wasudan wanaandamana mitaani wakitaka kuwaondowa waliofanya mapinduzi. Imekuweko miito iliyotolewa kupitia mitandaoni ya kuitisha maandamano haya makubwa leo Jumatano yakipewa jina tetemeko la ardhi la Aprili sita.
Jaafar Hassan, msemaji wa kundi la muungano wa kiraia unaopigania uhuru na mabadailiko-FFC ameyaita maandamano ya leo kuwa ni muhimu sana kwa Wasudan na kwamba Aprili ni mwezi wa Ushindi kwa umma wa Sudan. Viongozi wa muungano huo waliokuwa wakiuwakilisha upande wa kiraia katika serikali ya mpito waliondolewa kwenye nyadhifa zao kupitia mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba.
Mmoja wa waandamanaji,mjini Khartoum Badwi Bashir, amesema ni siku muhimu na wanatarajia watu wengi kujitokeza kwenye maandamano ya leo licha ya jua kali na Ramadhan kwasababu wanataka kuyamaliza mapinduzi na uwezekano wa kutokea tena mapinduzi nchini humo.Mtawala wa kijeshi Jenerali AbdulFatah al Burhani amesema anaweza tu kuyaachia madaraka ikiwa itapatikana taasisi ya kweli iliyochaguliwa na itakayokubaliwa na wasudan wote.
Sio tu mgogoro wa kisiasa lakini nchi hiyo hivi sasa inakabiliwa na hali ya mfumko mkubwa wa bei ya vyakula,mafuta na mahitaji muhimu tangu jeshi lilipotwaa madaraka. Uhalifu,ukosefu wa usalama umeongezeka katika maeneo ya vijijini na hasa katika jimbo la Darfur kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Wiki iliyopita kiasi watu 45 waliuliwa kufuatia mapigano makali kati ya wasudan wenye asili ya kiarabu na makabila mingine yasiyokuwa na nasaba ya uarabu huko Kusini mwa Darfur.