Maandamano yaendelea Tunisia
23 Januari 2011Waandamanaji hao kutoka mkoa masikini wa wakulima ambao ndio walichochea maandamano dhidi ya utawala wa kimabavu mwezi uliopita, wanataka kujiuzulu kwa serikali iliyochukua nafasi baada ya kuondolewa madarakani, Zine El Abidine Ben Ali.
Wakiandamana katikati mwa Tunis, waandamanaji hao wamesema wamekwenda kwenye mji huo kuiondoa madarakani serikali. Maandamano hayo ya ukombozi yalianza jana kwenye mji wa Menzel Bouzaiane, ambako mtu wa kwanza aliuawa katika maandamano ya kupinga utawala wa Ben Ali.
Kumekuwa na maandamano ya kila siku katika siku za hivi karibuni, kutaka kujiuzulu Waziri Mkuu Mohammed Ghannouchi, ambaye amekuwa katika wadhifa huo tangu mwaka 1999 na ameendelea kubakia madarakani, licha ya kuanguka kwa Ben Ali.
Waandamanaji hao pia wanataka kuvunjwa kwa kilichokuwa chama tawala cha RCD, ambacho kilitawala siasa za Tunisia kwa miongo kadhaa.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)
Mhariri: Hamidou, Oummilkheir