Maandamano yaendelea kuitikisa Iran
3 Januari 2018Maandamano hayo ambayo ndiyo makubwa zaidi kuikumba Iran tangu uchaguzi wake uliobishaniwa mwaka 2009, yameshuhudia siku sita za machafuko nchini Iran kote, na vifo vya watu wasiopungua 20.
Maandamano hayo yalianza Alhamisi wiki iliyopita katika mji wa Mashhad kupinga hali duni ya kiuchumi na kuongezeka kwa bei za vyakula, na yameenea katika miji kadhaa, huku baadhi ya waandamanaji wakiimba nyimbo za kuisokoa serikali na kiongozi wa juu Ayatollah Ali Khamenei.
Mamia ya watu wamekamatwa kuhusiana na maandamano hayo.
Televisheni ya Taifa imeripoti kuwa waandamanaji sita waliuawa wakati wa shambulizi kwenye kituo cha polisi katika mji wa Qahdarijan. Imeripoti kuwa makabiliano hayo yalisababishwa na waandamanaji waliojaribu kuiba silaba kutoka kituoni hapo.
Mvulana mwenye umri wa miaka 11 na mwanaume mwenye umri wa miaka 20 waliuawa katika mji wa Khomeinishahr, huku askari wa kikosi cha Ulinzi wa Jmahuri akiuawa katika mji wa Najafabad.
Ripoti hiyo ya televisheni ya Taifa inasema watatu hao waliuawa kwa kutumia silaha za uwindaji, ambazo hutumiwa kawaida katika maeneo ya mashamba nchini Iran.
Rais Rouhani ataka watu wapewe uhuru zaidi
Watu kumi walithibitishwa kuuawa nchini kote siku ya Jumatatu, wakati wimbi la maandamano hayo likiwa halionyeshi dalili ya kutulia, na kumlaazimu rais Hassan Rouhani na serikali yake kuzungumzia madai ya waandamanaji.
Katika ukosoaji usiyo wa moja kwa moja wa viongozi wenye msimamo mkali kwenye utawala, ambao wanapinga juhudi zozote za mageuzi ya kisiasa na kiuchumi, Rouhani alisema litakuwa kosa kubwa kuyaona maandamano hayo kama njama ya mataifa ya kigeni.
"Kwa mtazamo wangu, kilichotokea siku chache zilizopita, kinaweza kuonekana kwa juujuu kama kitisho, lakini tunahitaji kukigeuza kuwa fursa. Tunapaswa kuona tatizo ni nini," alisema rais Rouhani na kuongeza kuwa "siyo waandamanaji wote walioingia mitaani wamefuata maagizo kutoka mataifa mengine."
'Muda wa mabadiliko Iran'
Rais wa Marekani Donald Trump amtumia maandamano hayo kuishambulia mfululizo serikali ya Iran, na kuionya dhidi ya ukiukaji wowote wa haki za binadamu, akijengea kwenye vita vyake vya maneno dhidi ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 ambayo Iran ilisaini na mataifa makubwa chini ya mtangulizi wa Trump, Barack Obama.
Trump alisema katika mmoja ya jumbe zake alizoweka kwenye ukurasa wa Twitter kuwa, "wakati wa mabadiliko umewadia Iran."
Naye waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigma Gabriel, aliwataka maafisa wa serikali na waandamanaji pia kujiepusha na vitendo vyovyote vya vurugu, na kuitolea mwito serikali kuwaruhusu waandamanaji kupaza sauti zao kwa uhuru zaidi.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/Ape, Dpae, Afpe.
Mhariri: Grace Patricia Kabogo