1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yaendelea Hong Kong licha ya sherehe za kitaifa

Admin.WagnerD1 Oktoba 2014

Maelfu ya waandamanaji wanaotaka mageuzi ya kidemokrasia Hong Kong wameendelea kuandamana, huku wakimzomea kiongozi wa Hong Kong, Leung Chun Ying, alipokuwa akihudhuria sherehe za kuundwa kwa Jamhuri ya Watu wa China

https://p.dw.com/p/1DO9a
Picha: Reuters

Huku China ikiadhimisha miaka 65 tangu Chama cha Kikomunisti kuchukua madaraka na kutangaza Jamhuri ya Umma wa China tarehe mosi, mwezi Okotoba mwaka 1949, sherehe hizo zinagubikwa na maandamano makubwa ya kudai kutanuliwa kwa mfumo wa demokrasia na mageuzi ya sheria za uchaguzi Hong Kong.

Licha ya kuwa na mamlaka ya kujitawala chini ya mfumo wa serikali mbili, bado iko chini ya himaya ya China baada ya Uingereza iliyokuwa ikiitawala Hong Kong kuirejeshea China mwaka 1997.

Leung azomewa na waandamanaji

Maelfu ya waandamanaji ambao wameweka kambi katikati ya mji wa Hong Kong tangu Jumapili na kukwamisha shughuli za kibiashara na za serikali, wameghadhabishwa na kukataa kwa kiongozi wa Hong Kong kukutana nao.

Kiongozi wa Hong Kong Leung Chunying (Katikati) na viongozi wengine katika sherehe za taifa
Kiongozi wa Hong Kong Leung Chunying (Katikati) na viongozi wengine katika sherehe za taifaPicha: Reuters/Bobby Yip

Wakati wa ufunguzi wa sherehe hizo za China hii leo, waandamanaji hao wamemzomea Leung Chun Ying na kumtaka ajiuzulu kisha wakanyamaza na kugeuza migongo yao wakati helikopta zilizokuwa zimebeba bendera za China na Hong Kong zilipopita angani kama sehemu ya maadhimisho ya sherehe hizo.

Katika hotuba yake, Leung hakugusia moja kwa moja maandamano hayo ya kutaka mageuzi hasa kuhusiana na kufanyiwa marekebisho ya sheria za chaguzi ili kuruhusu kuwepo kwa uhuru zaidi wa kuwachagua viongozi katika uchaguzi unaotarajiwa mwaka 2017.

Leung amewaambia wapiga kura kuwa ni bora kukubaliana na mipango ya China ya kuwachuja na kuwateua wagombea wa uchaguzi kwani ndiyo mfumo bora.

Serikali ya kikomunisti ya China ambayo inaamini haiwezi kupingwa na lazima iendelee kutawala, imehakikisha hakuna taarifa zozote kuhusu maandamano hayo ya Hong Kong nchini China.

China yajikuta njia panda

Wachambuzi wanasema China inahofia kuwa kwa kulegeza kamba na kuitikia matakwa ya waandamanaji wa Hong Kong kutayapa makundi mengine ya wanaotaka kujitenga nguvu za kudai uhuru zaidi.

Rais wa China Xi Jinping akisherehekea miaka 65 ya utawala wa chama cha kikomunisti cha China
Rais wa China Xi Jinping akisherehekea miaka 65 ya utawala wa chama cha kikomunisti cha ChinaPicha: Getty Images/Feng Li

Maafisa wa China wamewakamata watu kadhaa nchini China na kuwahoji kiasi cha wanaharakati 60 ambao wameonyesha kuyaunga mkono maandamano ya Hong Kong.

Rais wa China Xi Jinping amesalia kimya kuhusu maandamano hayo lakini katika hotuba yake jana jioni kuadhimisha sherehe hizo za kitaifa zinazoanza rasmi hii leo, alisisitiza kuwa wanapaswa kutojitenga kamwe kutoka kwa watu.

Maandamano hayo ya Hong Kong ndiyo mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu China ichukue tena madraka juu ya Hong Kong kutoka kwa Uingereza na yanatoa changamoto kubwa mno ya kisiasa kwa Beijing juu ya namna ya kuyashughulikia tangu kuyakandamiza kwa nguvu kupita kiasi maandamano ya Tiananmen mwaka 1989.

Mwandishi: Caro Robi/ap/reuters/afp

Mhariri: Mohammed Khelef