Maandamano ya wanawake Afghanistan sasa hayafanyiki tena
6 Oktoba 2021Mikutano mingine iliyokuwepo awali ilisambaratishwa risasi za hewani vipigo kutoka kwa Taliban.
Upinzani ndani ya familia na wasiwasi kuhusu utoaji wa taarifa kupitia mitando ya kijamii inayoweza kuwatambua watu wanaoshiriki, pia vinakuwa kama vikwazo, kwa mujibu wa waandamanaji sita wanawake waliozungumza na shirika la habari la Uingereza Reuters.
Maandamano ya hapa na pale ya wanawake wanaolitaka kundi la Taliban kuheshimu uhuru wa wao wa kiraia, yalirushwa kwenye mitandao ya kijamii, kama ilivyokuwa kwa uitikiaji dhidi yake, ambao wakati mwingine ulikuwa wa vurugu, na kuvutia nadhari ya ulimwengu juu ya masuala ya usawa na haki za binadamu.
Waliovunja sheria waliadhibiwa kwa kupigwa hadharani
Mara ya mwisho Taliban ilipokuwa madarakani katika miaka ya 1990, liliwapiga marufuku wanawake kufanya kazi na wasichana kwenda shule. Wanawake waliruhusiwa tu kutoka nje wakiwa wameandamana na ndugu wa kiume na kusisitiza kwamba wanawake wavae navazi ya kufunika mwili mzima maarufu kama burqa.
Wale waliovunja sheria hiyo waliadhibiwa kwa kupigwa hadharani na wanachama wa kundi hilo waliojulikana kama "Polisi wa nmaadili"
Lakini kwa sasa kundi la Taliban limeahidi uhuru zaidi kwa wanawake ikiwemo katika masuala ya elimu na kazi kwa kuzingatia sheria za Kiislamu. Licha ya hayo bado wasichana wakubwa bado hawajarudi shule, hakuna wanawake katika nafasi za juu katika serikali mpya, wizara ya wanawake mjini Kabul imefungwa na Taliban tayari imesema kuwa wanawake watakubaliwa kufanya kazi katika idadi ndogo ya nafasi za kazi itakayokuwepo.
Wanawake sasa wanaotaka kuelezea hasira zao hadharani wanapambana kufanya hivyo. Sita walioshiriki maandamano baada ya Taliban kuchukua madaraka katikati ya mwezi Agosti, wamesema hawajaweza kuandamana tangu mwanzoni mwa mwezi Septemba.
Mmoja ya wanawake hao Nasima Bakhtiary, amesema wana mipango ya kuandaa maandamano zaidi lakini kutokana na sababu za kiusalama wanahofu ya kutoka nje maana wameshuhudia baadhi yao wakinyanyaswa.
Mapema mwezi huu kundi la Taliban lilisema halijapiga marufuku maandamano lakini wale wanaotaka kufanya hivyo ni lazima waombe idhini na kutoa taarifa za ndani zaidi ikiwemo, mahali, muda na maneno yatakayotumiwa katika maandamano hayo.
Kumekuwa na maandamano karibu 8 tangu Agosti 15
Hata hivyo msemaji wa kundi la Taliban hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo.
Kulingana na mahojiano na waandaaji wa maandamano, jumbe za mitandao ya kijamii na makundi ya wanaharakati, shirika la habari la Reuters limehesabu maandamano takriban 8 kuanzia Agosti 15 hadi tarehe 8 septemba, na kuanzia tarehe hiyo kumekuwa na maandamano mara moja tu yaliofanyika tarehe 19 Septemba nje ya wizara ya wanawake mjini Kabul baada ya kufungwa.
Maryam Sadat, msichana aliye na miaka 23, mwanafunzi wa sheria na mmoja ya waandaaji wa maandamano amesema yeye na wenzake walijaribu kuandaa maadnamano mengine tarehe 30 Septemba lakini yakavunjwa na wanachama wa Taliban.
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia haki za binaadamu, limelaani vurugu dhidi ya waandamanaji hasa wanawake. Taarifa kutoka katika shirika hilo imesema, waafghanistan wa kike na wa kiume wanapoandamana kwa amani wakati huu mgumu nchini mwao wakidai haki zao za binaadamu kuheshimiwa ni muhimu kwamba wale walio madarakani wanasikiliza sauti zao.