1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya wayahudi yazusha wasiwasi Jerusalem

15 Juni 2021

Serikali mpya ya Israel yakabiliwa na mtihani wa mapema wakati Mayahudi wenye msimamo mkali wanajiandaa kufanya maandamano makubwa katika ardhi ya Wapalestina iliyonyakuliwa kwa mabavu na Israel ya Jerusalem Mashariki.

https://p.dw.com/p/3uwUG
Israel Zusammenstöße auf dem Tempelberg am Jerusalemtag
Picha: picture-alliance/dpa/M. Illean

Serikali mpya ya Israel  inakabiliwa na mtihani wa mapema hii leo ambapo Mayahudi wenye msimamo mkali wanajiandaa kufanya maandamano makubwa katika ardhi ya Wapalestina iliyonyakuliwa kwa mabavu na Israel ya Jerusalem Mashariki.

Maandamano hayo makubwa  yanayopangwa kufanyika alasiri kwa saa za hapa Ulaya, yamezusha wasiwasi mkubwa na  Umoja wa Mataifa umetahadharisha kwamba yanatishia kuyaweka hatarini makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na Wapalestina kupitia kundi la Hamas ambayo ni tete.            

Maandamano hayo yanayoitwa maandamano ya kupeperusha bendera, kimsingi yanaadhimisha siku ya tukio la mwaka 1967 pale Israel ilipoinyakua kimabavu ardhi ya Jerusalem Mashariki. Awali yalikuwa yamepangwa kufanyika Alhamisi iliyopita  lakini yaliakhirishwa kutokana na kupingwa na polisi ya Israel na onyo lililotolewa na watawala wa Gaza, chama cha  Hamas.  

Israel | Jair Lapid und Naftali Bennett
Picha: JINI via Xinhua/picture alliance

Serikali ya Israel iliyokuweko wakati huo ya Benjamin Netanyahu iliyaakhirisha maandamano hayo hadi leo Jumanne, na  jana jumatatu usiku serikali mpya ya waziri mkuu Naftali Bennett  ikathibitisha juu ya kufanyika maandamano hayo hii leo.

Waziri wa mambo ya ndani Omer Bar-Lev akithibitisha kuhusu kufanyika maandamano hayo alisema na hapa namnukuu: "Haki ya kuandamana ni haki ya kila mmoja katika nchi zinazofuata demokrasia. Polisi iko tayari na tutafanya kila tunaloweza kulinda amani ya kila mmoja," mwisho wa kumnukuu.

Mikusanyiko ya makundi ya Mayahudi wenye misimamo mikali inayofanyika kwenye maeneo yanayokaliwa na Waarabu imeongeza hali ya  wasiwasi mkubwa na mivutano katika miezi ya hivi karibuni, na kusababisha polisi kuingilia kati katika eneo tete la Msikiti wa al Aqsa, tukio lililosababisha kuzuka machafuko makubwa ya umwagikaji damu kati ya Israel na Palestina ambayo hayajawahi kutokea tangu mwaka 2014.

Israel Zusammenstöße auf dem Tempelberg am Jerusalemtag
Picha: picture-alliance/dpa/M. Illean

Serikali imesema kwamba waandaaji wa maandamano haya ya leo wameshauriana na polisi kuhusu njia ya kupitisha maandamano hayo kuanzia alasiri kwa saa za Ulaya ya Kati, ili kuepusha malumbano na wakaazi wa Kiarabu kwenye eneo hilo.

Lakini Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Wapalestina, Mohammad Shtayyeh, amelaani hatua hiyo akisema ni uchokozi na kutoa tahadhari juu ya athari za hatari zinazoweza kusababishwa na nia ya Israel ya kuruhusu walowezi wa Kiyahudi kufanya maandamano hayo ya kupeperusha bendera katika eneo lililonyakuliwa kimabavu la Jerusalem.

Waziri Mkuu Shtayyeh ameongeza kusema kwenye ujumbe wake aliouandika kwenye mtandao wa twitta kwamba kitendo hicho cha Israel ni hatua ya kichokozi na kimabavu inayopaswa kukomeshwa dhidi ya Wapalestina, Jerusalem na maeneo yake matakatifu.

Ikumbukwe kwamba waziri mkuu mpya wa Israel binafsi ni Myahudi mwenye msimamo mkali lakini muungano wa serikali anayoiongoza unavijumuisha pia vyama vyenye msimamo wa wastani na vya siasa za mrengo wa shoto na kwa mara ya kwanza pia katika historia ya nchi hiyo kimo chama cha waarabu ndani ya muungano huo.

Bildkombo Israel mögliche neue Koalition Lapid
Picha: EMMANUEL DUNAND; THOMAS COEX; JACK GUEZ; MENAHEM KAHANA; AHMAD GHARABLI/AFP

Uungaji mkono wa wabunge wanne Waarabu kutoka chama cha kihafidhina cha Kiislamu cha Raam ulikuwa muhimu sana kwa Waziri Mkuu Naftali Bennet kumuwezesha kuwa na wingi mdogo uliomfanya kuunda serikali mpya na kumuondowa Netanyahu siku ya Jumapili iliyopita.

Maandamano ya leo yamezusha wasiwasi mpaka Umoja wa Mataifa ambapo mjumbe wa Umoja huo kuhusu Mashariki ya Kati, Tor Wennesland, amezitolea mwito pande zote kujizuia kuyaharibu makubaliano yaliyofikiwa kwa tabu Mei 21 na kumaliza mashambulizi makali ya siku 11 katika Ukanda wa Gaza yaliyochukua roho za Wapalestina 260 na huku Israel ikipoteza watu 12.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW