1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano New York kufuatia uamuzi wa kesi ya kuuawa kwa raia mweusi

4 Desemba 2014

Maelfu ya waandamanaji wameandamana katika mji wa New york nchini Marekani baada ya mahakama kutoa uamuzi kuwa askari aliyemuua raia mweusi kwa kumkaba koo hatafunguliwa mashitaka

https://p.dw.com/p/1Dz4A
Picha: ap

Punde baada ya mahakama kutangaza uamuzi huo wa kutomfungulia mashitaka askari mzungu Daniel Pantaleo aliyemuua mwanamume kwa jina Eric Garner mwenye umri wa miaka 43, mamia ya waandamanaji walikusanyika katika ukumbi wa rockefeller na katika ukumbi wa umma wa Newyork wakiimba hakuna haki hakuna amani.

Kamishna wa polisi wa mji wa Newyork Bill Bratton amesema wamewakamata watu thelathini.Makundi ya waandamanaji kutoka sehemu mbali mbali mjini humo walikutana kwa maandamano makubwa katika barabara kuu ya NewYork na gazeti la Washintgon Post limeripoti waandamanaji 5,000 wameandamana usiku wa kuamkia leo.

Garner alikufa mikononi mwa polisi akikamatwa kwa kuuza sigara ambazo zilikuwa hazijalipiwa kodi na hakuwa na silaha wakati wa tukio hilo lililotokea mwezi Julai mwaka huu.

Uchunguzi mpya kuanzishwa

Kufuatia uamuzi huo wa mahakama,Mwanasheria mkuu wa Marekani Eric Holder amesema ofisi yake itaanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha Garner baada ya kukabwa koo na askari.

Rais wa Marekani Barack Obama na Mwanasheria mkuu Eric Holder
Rais wa Marekani Barack Obama na Mwanasheria mkuu Eric HolderPicha: Reuters/Gary Cameron

Tangazo hilo la Holder linamaanisha kuna uwezekano askari anayetuhumiwa akachukuliwa hatua.Video iliyonakiliwa wakati Garner akikamatwa na askari kadhaa inaonyesha akisema mara kadhaa kuwa hawezi kupumua baada ya kuwekwa chini na askari akiwa amebanwa kooni.

Rais wa Marekani akizungumza muda mfupi baada ya uamuzi wa mahakama amesema kuuawa kwa Garner sio tatizo la watu weusi au weupe bali la Marekani nzima.

Askari wazungu wadaiwa kuwalenga raia weusi

Hayo yanakuja baada ya uamuzi wa mahakama ya Fergusson katika jimbo la Missouri kutomshitaki askari aliyemuua kijana wa miaka 18 Michael Brown mwezi Agosti uamuzi ambao ulisababisha maandamano makubwa nchini humo kupinga ubaguzi wa rangi.

New York USA Proteste 4.12. Eric Garner
Waandamanaji wakiandamana New York kupinga mauaji ya Eric GarnerPicha: Reuters/Stephen Lam

Askari wazungu wameshutumiwa na jamii ya watu weusi nchini Marekani kwa kutumia nguvu kupita kiasi wanaposhughulikia visa vinavyowahusisha washukiwa weusi.

Askari Pantaleo amesema anaiombea familia ya Garner na anatumai watakubali rambi rambi zake.Hata hivyo mjane wa Garner Esaw Garner amesema hakubali radhi kutoka kwa Pantaleo na kusema wakati wa kuonyesha majonzi na kujuta ulikuwa wakati mumewe alikuwa amelazwa chini akisema hawezi kupumua.

Meya wa Newyork De Blasio amesema maafisa wa Marekani wanapaswa kushughulikia ukweli wa mambo kuhusu ubaguzi wa rangi ambao nchi hiyo imekuwa ikabiliana nayo kwa karne kadhaa.

Mwanaharakati wa kutetea haki za raia Al Sharpton amewataka watu kujitokeza kwa wingi hii leo kuandamana mjini washington kupinga uamuzi huo wa mahakama.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Ap

Mhariri: Josephat Charo