Maandamano nchini Zimbabwe.
15 Aprili 2008HARARE.
Majeshi yamewekwa tayari nchini Zimbabwe kote wakati maandamano yaliyoitishwa na chama cha upinzani yanatarijiwa kuanza kufanyika leo nchini humo.
Chama cha upinzani MDC kimeitisha maandamano hayo kupinga uamuzi wa mahakama kuu ya Zimbabwe kutupilia mbali rufaa ya chama hicho juu ya kuitaka mahakama hiyo iiamrishe tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya uchaguzi uliofanyika zaidi ya wiki mbili zilizopita nchini zimbabwe.
Jaji wa mahakama kuu hiyo amesema matokeo ya uchaguzi hayatatangazwa mpaka taarifa juu ya kosoro zilizojitokeza katika kupiga kura zitakapochunguzwa.
Lakini makamu mwenyekiti wa chama cha MDC Thokozani Khupe amesema maandamano yatafanyika
mpaka hapo matokeo ya uchaguzi yatakapotangazwa.
Wakati huo huo chama cha upinzani MDC kimesema kuwa matendo ya kutumia nguvu yameenea nchini. Chama hicho kimefahamisha kuwa msimamizi wake mmoja wa uchaguzi ameuliwa na wanamgambo wa chama cha Mugabe ZANU- PF.
Na habari zaidi zinasema kuwa Marekani na Uingereza zinakusudia kuliwasilisha suala la Zimbabwe kwenye baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo kesho licha ya upinzani wa Afrika Kusini.