Maandamano makubwa tena Hong Kong
16 Juni 2019Sheria hiyo inayopendekezwa imezusha hofu ya kupanuliwa udhibiti wa serikali ya mjini Beijing katika koloni hilo la zamani la Uingereza.
Waandamanaji wanadai kwamba kiongozi wa Hong Kong aufute kabisa mswada wa kusafirishwa kwenda China bara ambao utaruhusu baadhi ya watuhumiwa kupelekwa kwa ajili ya kushitakiwa katika China bara na kisha ajiuzulu. Mzozo huo , ambao ulitumbukia katika ghasia kubwa na polisi wiki iliyopita, ni moja kati ya mtihani mkubwa wa hadhi maalum ya eneo hilo tangu China kuchukua udhibiti baada ya kukabidhiwa mwaka 1997.
Waandamanaji walibeba mabango yanayodai kuwa mtendaji mkuu Carrie Lam ajiuzulu na hilo likawa kauli mbiu iliyokuwa ikiimbwa mara kwa mara na waandamanji. Wakitembea taratibu na kuimba "ondoa" na jiuzulu," kundi hilo la watu waliijaza bara bara kuu pamoja na eneo la pembeni yake mkabala na eneo la maji la bandari ya Victoria wakati watalii na wanunuzi ambao hutembelea sehemu hiyo ya kitovu cha biashara na fedha katika eneo la asia wakiangalia.
Tangazo la Lam siku ya Jumamosi kuwa anasitisha sheria hiyo limeshindwa kuwatuliza wakosoaji wa hatua hiyo ambao wanaiona kuwa moja katika hatua ambacho zinakula uhuru wa Hong Kong pamoja na sheria ya mamlaka yake ya ndani.
Hofu ya wapinzani
Wapinzani wanahofu kwamba sheria hiyo inaweza kutumika kuwapeleka watuhumiwa wahalifu nchini China na kuwa na uwezekano wa kukabiliwa na mashitaka yasiyoeleweka ya kisiasa, uwezekano wa kufanyiwa mateso na hukumu kinyume na haki.
"Madai yetu ni rahisi. Carrie Lam lazima aondoke madarakani, sheria ya kupelekwa China bara ni lazima iondolewe na polisi wanapaswa kuomba radhi kwa kutumia nguvu kubwa dhidi ya watu wake," mfanyakazi wa benki John Chow amesema wakati akiandamana pamoja na kundi la marafiki zake. "Na tutaendelea."
Maandamano hayo ya Jumapili (16.06.2019) yanaonekana kuwa katika kiwango sawa na wiki moja iliyopita ambayo yaliwaleta pamoja kiasi ya watu milioni moja wakielezea wasi wasi wao kuhusiana na uhusiano wa Hong Kong na China bara. Waandamanaji walilenga hasira zao kwa Lam, licha ya kukiri kwamba hana uchaguzi lakini kuendelea kupokea maelekezo yanayotolewa na Beijing, ambako rais Xi Jinping ameimarisha utawala wa mkono wa chuma.
Wengi hapa wanaamini haki ya mamlaka ya Hong Kong imepunguzwa kwa kiasi kikubwa licha ya msisitizo kutoka Beijing kwamba bado inatimiza ahadi yake, inayofahamika kama "nchi moja , mifumo miwili," kwamba eneo hilo linaweza kuendelea na mfumo wake wa kijamii, kisheria na kisiasa kwa miaka 50 baada ya kukabidhiwa China kutoka Uingereza.