1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano makubwa dhidi ya Wahouthi Yemen

24 Januari 2015

Maelfu ya wananchi wa Yemen wameingia mitaani Jumamosi(24.01.2015) katika maandamano makubwa kabisa dhidi ya kundi la Wahouthi lenye kuidhibiti Yemen siku mbili baada ya kujizulu kwa Rais Abd-Raboo Hadi.

https://p.dw.com/p/1EQ37
Waandamanaji wanaopinga Wahouthi Sanaa .(24.01.2015)
Waandamanaji wanaopinga Wahouthi Sanaa .(24.01.2015)Picha: Reuters/M. al-Sayaghi

Mashahidi wanasema umma wa watu wanaokadiriwa kufikia 10,000 waliandamana kutoka Chuo Kikuu cha Sanaa na kuelekea makaazi ya Rais Hadi kwenda na kurudi kama kilomita tatu hivi wakirudia kutowa mayowe wakishutumu makundi yote mawili la madhehebu ya Shia la Wahouthi na lile la Wasunni la Al Qaeda.

Umma huo umekuwa ukipiga mayowe "Wadumu wananchi wa Yemen.Hapana kwa Wahouthi na hapana kwa Affash" jina la utani la Rais wa zamani wa nchi hiyo Ali Abdullah Saleh ambaye alipinduliwa hapo mwaka 2011 katika uasi wa umma dhidi ya utawala wake wa miaka 33.

Saleh ametajwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuwasaidia Wahouthi kuiteka Sanaa ambao ni mji mkuu wa nchi hiyo yenye idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Sunni hapo mwezi wa Septemba.

Hadi awalaumu Wahouthi

Rais Hadi ambaye alijiuzulu hapo Alhamisi alilaumu kudhibitiwa kwa mji wa Sanaa na Wahouthi kuwa kunakwamisha juhudi zake kuingoza nchi hiyo kwenye utulivu baada ya miaka kadhaa ya machafuko, umaskini ulioota mizizi na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Marekani kwa wanamgambo wa itikadi kali Waislamu wa madhehebu ya Sunni.

Rais wa Yemen aliyejiuzulu Abd-Rabbu Mansour Hadi.
Rais wa Yemen aliyejiuzulu Abd-Rabbu Mansour Hadi.Picha: Reuters

Wahouthi walikuwa wakimshikilia Hadi kama mfungwa nyumbani kwake wiki hii.Wanamshutumu kwa kukengeuka makubaliano ya kushirikiana madaraka waliyosaini na vyama vikuu vya kisiasa nchini humo mbele yake baada ya kuuteka mji wa Sanaa.

Mmojawapo wa wanafunzi aliyejitambulisha kwa jina la Maimouna aliyekuwa amebeba bango lenye kupinga mipango ya kuwajumuisha jeshini wapiganaji wa Houthi amekaririwa akisema "Tumejitokeza leo kupinga mapinduzi na kupinga udhibiti wa Wahouthi kwa mji mkuu."

Wahouthi wazomewa

Waandamanaji walizuwiya magari mbele ya makaazi ya Rais Hadi na kuwazomeya wapiganaji wa Kihouthi walioko katika eneo hilo na kuwapigia makelele "Ondokeni Wahouthi, ondokeni ".

Waandamanaji wakikabiliana na wafuasi wa Wahouthi Sanaa.(24.01.2015).
Waandamanaji wakikabiliana na wafuasi wa Wahouthi Sanaa.(24.01.2015).Picha: Reuters/M. al-Sayaghi

Wapiganaji hao Wahouthi waliwazuwiya waandamanaji kuikaribia nyumba ya Rais Hadi lakini walijatahidi pamoja na polisi kuwa mbali nao.

Maadamano kama hayo yalifanyika katika majimbo mengine ikiwa ni pamoja na Taiz,Hodeida,al - Bayda na Ibb.

Hatari ya nchi kugawika

Hapo Ijumaa maelfu ya wafuasi wa Wahouthi walikusanyika mjini Sanaa wakiwa na mabango yenye kutowa wito wa "Kifo kwa Marekani,Kifo kwa Israel" ambayo imekuja kuwa mojawapo ya kauli mbiu yao.

Wakati kukiwa hakuna serikali kuu huko Sanaa maafisa wa serikali za mitaa katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo wametangaza kwamba hawatopokea tena amri kutoka mji mkuu huo na hiyo na kuzusha hofu kwamba nchi hiyo inaweza kugawanyika.

Mpiganaji wa kundi la Wahouthi.
Mpiganaji wa kundi la Wahouthi.Picha: Reuters/Abdullah

Maazimio kama hayo yametoka katika majimbo ambayo hapo zamani yalikuwa yameunda Yemen Kusini ambapo vuguvugu la kutaka kujitenga limekuwa likidai uhuru na jimbo la Marib lenye utajiri wa mafuta lilioko mashariki ya Sanaa.

Bunge la Yemen linatarajiwa kukutana Jumapili kujadili kujiuzulu kwa Hadi.Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo spika wa bunge Yahya al- Ra'i ambaye anatokea chama cha GPC cha Saleh anatakiwa kushika madaraka ya kipindi cha mpito wakati uchaguzi mpya ukiandaliwa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri : Amina Mjahid