1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano kufanyika Misri licha ya kitisho cha serikali

MjahidA30 Agosti 2013

Chama cha Udugu wa Kiislamu kimepanga kuandamana baada ya sala ya Ijumaa dhidi ya serikali ya mpito nchini humo. Maandamano hayo yameitishwa licha ya serikali kutishia kutumia nguvu kupambana na waandamanaji.

https://p.dw.com/p/19YxG
Maandamano Misri
Maandamano MisriPicha: picture-alliance/dpa

Maandamano haya ya leo yanatarajiwa kupima ni kwa kiwango gani vikosi vya usalama vimelidhoofisha kundi hilo na hii itajulikana tu kwa namna watu watakavyojitokeza katika maandamano hayo.

Kulingana na wakaazi huko, maandamano ya leo yanahofiwa kuzua machafuko zaidi katika nchi hiyo iliyokumbwa na msukosuko wa kisiasa.

Umwagikaji mkubwa wa damu ulishuhudiwa wiki mbili zilizopita baada ya polisi kushambulia kambi za waandamanaji waliokuwa wanapinga hatua iliyochukuliwa Julai 3 ya kumuondoa madarakani kiongozi wao Mohammed Mursi kwa njia ya mapindzi ya kijeshi.

Maandamano Misri
Maandamano MisriPicha: Reuters

Hali hiyo ilisababisha vurugu ya wiki nzima zilizowauwa watu takriban 1,000, wengi wao wakiwa wafuasi wa Mursi. Inadaiwa kuwa baadhi ya wafuasi hao walijibu mashambulizi kwa kuchoma makanisa, majengo ya serikali na pia kushambulia vituo vya polisi.

Pande zote mbili zaombwa kusuluhisha tofauti zao

Katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press, kiongozi wa kundi lililokuwa la waasi la Gamaa Islamiya, Abboud el-Zommor, alizihimiza pande zote mbili serikali na upinzani kukaa pamoja na kutatua tofauti zao ili kusimamisha umwagikaji wa damu nchini humo.

Huku hayo yakiarifiwa serikali imeongeza majeshi yake katika maeneo tofauti nchini humo huku ikilishutumu kundi la Udugu wa Kiislamu kuitisha maandamano na kuzua ghasia.

Wakati huo huo utawala wa Misri umeendelea kuwakamata viongozi wa kundi hilo kwa madai ya kuchochea ghasia. Tayari viongozi wawili, Mohammed el-Beltagy na Khaled el-Azhari, walikamatwa hapo jana.

Kiongozi wa Udugu wa Kiislamu Mohamed El-Beltagi
Kiongozi wa Udugu wa Kiislamu Mohamed El-BeltagiPicha: Reuters

Polisi wanasema waliwakamata kwa sababu ya kuchochea maandamano na kuteswa kwa polisi aliyekamatwa na waandamanaji mjini Cairo.

Kwa upande wake. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imesema itapambana vikali na watu ambao wanajaribu kuyumbisha usalama wa nchi na kwamba polisi wamepewa amri ya kutumia nguvu katika kulinda mali ya umma na ile ya watu binafsi nchini humo.

Wizara hiyo imesema pia kuwa maandamano ya leo yana lengo la kusababisha vurugu.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AP

Mhariri: Mohammed Khelef