Maandamano hayajasita Uturuki
11 Juni 2013Hatua hiyo ya polisi inakuja muda mfupi tu baada ya waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kukubali kukutana na waandalizi wa maandamano hayo ambayo wiki mbili tu zilizopita yalinuiwa kuwa ya amani kupinga mradi wa serikali wa ujenzi katika bustani ya Gezi lakini badala yake yamegeuka kuwa maandamano dhidi ya utawala wake.Watu watatu wameuawa na wengine 5,000 wamejeruhiwa kwenye maandamano hayo.
Polisi hao wamesema wanataka tu kuondoa mabango na kuusafisha mji huo na wala si kuwatawanya waandamanaji waliokita kambi katika bustani ya Gezi.Gavana wa Istanbul Huseyin Avni Mutlu ameandika kwenye akaunti yake ya twitter kuwa nia yao ni kuondoa mabango na picha zilizowekwa katika eneo la kihistoria lililo na sanamu ya kiongozi wa zamani wa Uturuki Mustafa Kemal Ataturk.
Moshi ulitanda katika ukumbi huo huku polisi wakirusha mabomu ya kutoa machozi na kuwahimiza waandamanaji hao kuwa watulivu na kurejea katika bustani ya Gezi.Baadhi ya waandamanaji hao walianza kuwarushia mawe na vitu vingine maafisa hao wa polisi.
Erdogan alegeza msimamo
Erdogan amekuwa akiwapuuza waandamanaji hao na kuwaita walala hoi lakini naibu waziri mkuu Bulent Arinc hapo jana alisema viongozi wa waandamanaji hao wametaka kukutana na waziri mkuu katika juhudi za kumaliza machafuko hayo ya karibu wiki mbili.Mkutano umepangiwa hapo kesho.
Maandamano hayo yametia doa hadhi ya taifa hilo lenye waislamu wengi ambalo linajisifia demokrasia dhabiti katika kanda ambayo inakumbwa na msukosuko na kama soko linaloinukia kwa kasi kwa wawekezaji.
Matumizi ya nguvu kupita kiasi ya polisi dhidi ya waandamanaji yamezua shutuma kutoka mataifa ya magharibi na Erdogan amekuwa akilaumu muingilio wa kigeni kwa kuchochea hali nchini humo.
Waandamanaji hao wamekuwa wakifanya maandamano licha ya vitisho kutoka kwa waziri mkuu huyo kuwa watajipata matatani kwa kutoiheshimu serikali yake.Siku ya Jumapili alionekana kuchochea uasi dhidi yake kwa kufanya mikutano ya hadhara iliyohudhuriwa na wafuasi wa chama chake cha AKP.
Waandamanaji hawatetereki
Wanaompinga wanamshutumu Erdogan kwa kuwakandamiza wakosoaji wake wakiwemo wanahabari,watu kutoka jamii ndogo ya wakurdi na jeshi na kujaribu kushinikiza ajenda za kidini katika taifa hilo ambalo licha ya kuwa na waislamu wengi haliendeshwi kwa misingi ya kidini.
Licha ya uasi huo dhidi yake; Erdogan mwenye umri wa miaka 59 anachukuliwa kuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa sana tangu Mustafa Kemal Ataturk anayetajwa baba wa Uturuki mambo leo na ambaye mpaka sasa anasalia kiongozi anayenziwa mno nchini humo.
Mwandishi: Caro Robi/afp /reuters
Mhariri: Josephat Charo