1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano dhidi ya Marekani yapamba moto

Admin.WagnerD14 Septemba 2012

Maandamano ya kupinga filamu inayokashifu dini ya kiislamu na mtume wake Muhammad yanaendelea kwenye nchi za kiarabu. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amelaani filamu hiyo ambayo ameiita ni ya chuki.

https://p.dw.com/p/168pI
Ägypten Proteste vor der US Botschaft in KairoPicha: AP

Naye mpinzani wa Rais Barack Obama kwenye uchaguzi wa urais Novemba mwaka huu, Mitt Romney, amekosoa namna serikali ya Marekani inavyoshughulikia mauwaji ya maafisa wake wa ubalozi.

Zaidi ya waandamanaji 200 wamejeruhiwa katika maandamano yanayoendelea kwenye ubalozi wa Marekani mjini Cairo Misri kupinga kudhalilishwa kwa Mtume Muhammad kupitia filamu iliyotengenezwa nchini Marekani.

Polisi wamemwagwa kwenye eneo lililo karibu na uwanja wa Tahrir wakifyatua mabomu ya machozi dhidi ya waandamanaji ambao wanarusha mawe. Kituo cha televisheni cha taifa kimeinukuu wizara ya afya ikisema kuwa watu 224 na askari 31 wamejeruhiwa katika vurugu hizo.

Maandamano mjini Cairo, Misri kupinga filamu inayomkashifu Mtume Muhammad
Maandamano mjini Cairo, Misri kupinga filamu inayomkashifu Mtume MuhammadPicha: AP

Yasambaa nchi zingine

Maeneo mengine ambayo maandamano yameendelea kufanyika ni pamoja na Libya, Yemen, Lebanon na Iran. Hii leo pia Sudan imetangaza kufanya maandamano makubwa baada ya sala ya Ijumaa kupinga filamu hiyohiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amelaani kitendo cha kutengenezwa kwa filamu hiyo aliyoiita ya chuki ambacho kimesababisha vifo vya balozi wa Marekani nchini Libya, Christopher Stevens, pamoja na afisa habari wa ubalozi huo, Sean Smith.

Watu wengine wawili waliouawa kwenye mashambulizi hayo wametambuliwa kuwa ni Tyrone Woods na Glen Doherty, wanajeshi wa zamani wa vikosi vya majini waliokufa wakijaribu kuwaokoa wenzao.

Rais Barack Obama na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton
Rais Barack Obama na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary ClintonPicha: Getty Images

Ban ametoa wito wa kuwepo na utulivu, uvumilivu na kusisitiza kuwepo mazungumzo ya amani katika kutatua suala hilo. Awali Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, alilaani pia filamu hiyo na kusema Marekani haihusiki kwa namna yoyote katika utengenezaji wake.

"Serikali ya Marekani haihusiki hata kidogo na filamu hiyo. Tunakemea kwa nguvu maudhui na kila kilichomo kwenye filamu hiyo. Uvumilivu wa Marekani kwenye masuala ya dini uko tangu mwanzoni kabisa wa taifa letu na kama unavyojua sisi ni nchi ya watu wa dini zote" ,alisema Bbibi Clinton.

Kauli ya Romney

Kitendo cha Rais Barack Obama na Clinton kulaani filamu hiyo kimemkasirisha Mitt Romney ambaye ameukosoa utawala wa Marekani kwa namna unavyoshughulikia suala hilo. Akiwa kwenye kampeni zake Virginia kaskazini, Romney amesema kuwa sasa inaonekana kuwa mhurumiaji wa dunia na kutaka kuwepo kwa jeshi imara zaidi la nchi hiyo. Amemtuhumu Obama kuwa anawaomba radhi maadui wa Marekani badala ya kulaani mauwaji.

Hata hivyo kauli hiyo ya Romney imepata upinzani sio tu kutoka kwa wafuasi wa chama cha Democratic bali pia wenziwe wa chama cha Republican. Wachambuzi wanasema kuwa Romney alikurupuka kutoa kauli kama hizo katika wakati usiofaa kwani Obama na Clinton wote wamelaani mauwaji hayo.

Mitt Romney, mgombea Urais wa Chama cha Republican, Marekani
Mitt Romney, mgombea Urais wa RepublicanPicha: Getty Images

Rais Obama mwenyewe amesema kuwa Romney ni mzuri wakukimbilia kufyetua risasi na kisha baadaye kulenga shabaha na kuongeza kuwa mtu wa aina hiyo hafai kuwa rais wa taifa kama Marekani.

Mwandishi: Stumai George/DPA/AFP/Reuters

Mhariri:Josephat Charo