Maandamano Armenia baada ya Pashinyan kukataliwa na bunge
2 Mei 2018Waandamanaji wakiwemo wazee wamekwamisha shughuli za kawaida katika mji wa Yerevan, huku karibu barabara zote, maduka, usafiri wa treni na barabara kuelekea katika uwanja wa ndege pia zikifungwa.
Waandamanaji hao wameapa kusalia barabarani hadi pale utawala wa nchi hiyo utakaapondoka madarakani na kumruhusu Pashinyan kuwa Waziri mkuu.
Maandamano kote nchini yaitishwa
Kiongozi huyo wa upinzani amewataka Warmenia kuendelea kuandamana dhidi ya chama tawala cha Republican baada ya uteuzi wake wa kuwa waziri mkuu kupingwa bungeni jana.
Bunge lilipiga kura 55 dhidi ya 45 kumpinga Pashinyan kuchukua wadhifa huo. Chama hicho cha Republican kinachoongozwa na Serzh Sarkisyan kimesema mhariri huyo wa zamani wa magazeti siyo mgombea anayestahiki kuchukua wadhifa wa waziri mkuu.
Pashinyan ana uungwaji mkono wa vyama vya upinzani ambavyo kwa jumla vina viti 47 katika bunge lenye wabunge 105. Anahitaji wingi wa kura ili kuidhinishwa kuwa waziri mkuu.
Punde baada ya kura hiyo bungeni, Pashinyan amesema watawala waliotangaza vita dhidi ya watu wake wamejiangamiza kisiasa akisisitza kuwa hakuna mtu anayeweza kuchukua ushindi kutoka kwa umma.
Eduard Sharmazanov, naibu wa spika wa bunge na msemaji wa chama cha Republican amesema Pashinyan ni mtu asiyetabirika.
Taifa hilo limekumbwa na mzozo wa kisiasa kwa zaidi ya wiki mbili baada ya Pashinyan kuongoza maandamano makubwa ya umma kumuondoa madarakani Serzh Sarkisian, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyehudumu kwa miaka kumi hadi Machi mwaka huu alipoteuliwa na bunge kuwa waziri mkuu, jambo ambalo liliwaghadhabisha raia wa nchi hiyo ambao walimuona kama kiongozi anayetaka kung'angania madaraka.
Bunge kuvunjwa iwapo Waziri mkuu hatateuliwa
Pashinyan amewasilisha tena azma yake ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu baada ya jaribio la kwanza kushindwa bungeni akiahidi kuendelea na uasi wa kiraia, kupitia maandamano na kuongeza watatafakari na kufanya majadiliano bila ya kuvunjika moyo katika azma yao ya kuiongoza Armenia.
Iwapo bunge litashindwa kwa mara ya pili kumteua waziri mkuu, litavunjwa na chaguzi za mapema kuitishwa. Pashinyan amesema iwapo hilo litatotokea, basi mojawapo ya hatua vuguvugu lake litachukua ni kususia chaguzi.
Hapo jana, alionya kuwa kushindwa kwa wabunge kumchagua kuwa waziri mkuu kutapelekea kile alichokitaja gharika ya Tsunami. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 42 anasisitiza kuwa ndiye kiongozi pekee nchini humo anayeweza kupambana dhidi ya ufisadi, umaskini na kusimamia chaguzi huru na za haki.
Wachambuzi na jumuiya ya kimataifa wanatiwa wasiwasi na mzozo unaojiri nchini humo kuwa huenda ukasababisha msukosuko katika taifa hilo lililokuwa chini ya utawala wa Kisovieti, na mshirika wa karibu wa Urusi.
Maafisa wa Urusi wanafuatilia kwa karibu yanayojiri Armenia kuona kama siasa za nchi hiyo zitachukua mkondo wa Georgia na Ukraine ambako maandamano ya umma yalipelekea uongozi mpya wa viongozi ambao waliziondoa nchi zao kutoka uhusiano wa karibu na Urusi.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp/ap
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman