Maandalizi ya Olimpiki yakabiliwa na changamoto
29 Februari 2016Kutoka kwa mlipuko wa virusi vya Zika hadi uchafuzi mkubwa wa maji, kutoka kwa maeneo na viwanja ambavyo havijakamilika vizuri hadi usafiri wa kuchelewa wa matreni, kutoka kwa mauzo ya chini ya tiketi hadi kupunguzwa kwa huduma, kutoka kwa uchumi unaodorora hadi kitisho cha kura ya kutokuwa na imani na rais wake, msisimko wa michezo hiyo ya kwanza kabisa kuandaliwa Amerika Kusini yanakabiliwa na orodha ndefu ya matatizo.
Maandalizi ya mwisho ya michezo ya Rio na hali ya juhudi za kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu nchini Urusi na Kenya vitakuwa mada kuu wakati bodi ya kuu ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki itaandaa mkutano wa siku tatu kuanzia kesho mjini Lausanne, Uswisi.
Bodi hiyo inatarajiwa kujadili hatua zilizopigwa katika kuwatambua wanamichezo ambao ni wakimbizi ambao watashindana chini ya bendera ya IOC mjini Rio, pendekezo la kuundwa shirika huru la kushughulikia suala la kuwafanyia wanariadha vipimo vya dawa za kuongeza nguvu, na mipango ya Mahakama ya Usuluhisi wa migogoro ya michezo kusimamia adhabu za wanaopatikana na hatia ya kutumia dawa hizo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP
Mhariri: Mohammed Khelef