Maafisa wahukumiwa kwa uzembe Afghanistan
19 Mei 2015Hukumu hiyo imetolewa baada ya wanaume wanne wa Aghanistan kuhukumiwa kifo, huku wengine wanane wakihukumiwa miaka 16 jela mapema mwezi huu kwa mauaji ya mwanamke huyo kwa jina Farkhunda aliyekuwa na miaka 27.
"Mmehukumiwa kutokana na uzembe wa majukumu yenu, mwaka mmoja jela," alisema jaji Safiullah Mojaddidi kwa washitakiwa hao 11 waliojumuisha maafisa wakuu wa polisi. Hata hivyo maafisa wengine wanane hawakupatikana na hatia. " Uamuzi huu sio wa mwisho washitakiwa wana haki ya kukata rufaa," aliongeza jaji Safiullah Mojaddidi.
Kundi la watu waliojaa hasira walimshambulia Farkhunda tarehe 19 mwezi Machi, kwa kumpiga vibaya na kumchoma moto karibu na mto Kabul. Baada ya tukio hilo watu 49 walikamatwa wakiwemo maafisa 19 wa polisi.
Kutokana na mikanda ya video iliochukuliwa na watu waliokuwa karibu, polisi hao walionekana wakisimama tu katika eneo la tukio bila kuchukua hatua zozote za kulizuwiya kundi hilo kumpiga Farkhunda.
Shambulizi hilo lilitokea baada ya muuzaji mikufu alipomtuhumu Farkhunda kimakosa kuchoma kitabu cha Koran. Mauaji yake yalisababisha maandamano nchini Afghanistan na kuzua hisia mbali mbali duniani juu ya namna wanawake wa Afghanistan wanavyodhulumiwa.
Mchakato wa kuendesha kesi hizo wakosolewa
Licha ya kupongezwa hukumu hizo za kwanza za aina hiyo nchini Afganistan pia kulikuwa na wasiwasi juu ya usawa wake. Kwa upande wake shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch lilisema linawasiwasi juu ya namna kesi hizo zilivyoendeshwa kwa kuwa wengi wa washitakiwa walikosa mawakili wa kuwawakilisha.
Awali Heather Barr, mtafiti mkuu katika shirika moja la kutetea haki za wanawake barani Asia, amesema kesi hii inatoa hisia kwamba serikali ya Afghanistan inataka kufanyika mchakato wa haraka wa kuitoa kesi hii nje ya vyombo vya habari na kusonga mbele, badala ya kuishughulikia ipasavyo na kuchunguza kwa haki ni kwa namna gani tukio kama hili linaweza kutokea.
Kesi hii ya Farkhunda inaangazia hali ya ukatili inayoendelea kwa wanawake wa Aghanistan licha ya mabadiliko kufanywa tangu utawala wa Taliban ulipoanguka mwaka wa 2001.
Wakati huo huo ripoti ya Umoja wa Mataifa imeihimiza serikali ya nchi hiyo kuimarisha upatikanaji wa haki kwa waathiriwa wa kike wanaopitia ukatili.
Kwa sasa kesi nyingi za ukatili dhidi ya wanawake zinasuluhishwa kupitia upatanishi hii ikionyesha mapungufu yaliopo katika mfumo wa makosa ya jinai ikiwemo madai ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Mwandishi Amina Abubakar/ afp/dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman