1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wa soka Nigeria washitakiwa kwa kutumia fedha vibaya

19 Oktoba 2018

Maafisa 3 wa soka nchini Nigeria wameshitakiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya fedha

https://p.dw.com/p/36oVE
Nigerianische Fußball-Nationalmannschaft
Picha: Imago/East News

Maafisa watatu wa soka nchini Nigeria wameshitakiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya kiasi cha dola milioni 9.5 za msaada kutoka kwa shirikisho la soka duniani, FIFA ambazo walizitumia kwa manufaa yao binafsi.

Tume ya kupambana na ufisadi nchini humo, EFCC imesema kwenye taarifa yake kwamba maafisa hao Christopher Andekin, Jafaru Fadanari Mamza na Rajan Zaka wanadaiwa kufanya kosa hilo mwaka 2015.

Limesema fedha hizo za msaada zilizotolewa na FIFA, zililenga kuimarisha soka nchini humo. Mwanasheria wa EFCC Steve Odiase aliwaambia waandishi wa habari nje ya mahakama ya juu ya Nigeria, mjini Abuja kwamba shauri hilo limeahirishwa hadi litakaposikilzwa tena Novemba 28.

Msemaji wa shirikisho la soka nchini humo Wilson Uwujaren, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watuhumiwa hao wamekana kosa hilo na walipewa dhamana kwa sharti la kuwasilisha pasi zao za kusafiria na kulipa naira mioni 5.