Maafisa 63 wa usalama na jeshi watiwa mbaroni Ethiopia
13 Novemba 2018Miongoni mwa waliokamatwa ni mkuu wa zamani wa kampuni kubwa ya kijeshi ya uhandisi na utengenezaji chuma METEC. Kukamatwa kwa maafisa hao wa ngazi ya juu ni matokeo ya uchunguzi wa miezi mitano ulioagizwa na kiongozi wa taifa hilo la Mashariki mwa Afrika anayelenga kuleta mageuzi Abiy Ahmed.
Mwanasheria mkuu wa Ethiopia Berhanu Tsegaye aliwaambia waandishi wa habari jana Jumatatu kwamba "jumla ya watu 36 walikamatwa kutokana na kushiriki kwenye ukiukwaji wa haki za binadamu huku wengine 27 wakikamatwa kwa madai ya rushwa".
Madai hayo ya ukiukwaji wa haki za binadamu yalisababisha uonevu dhidi ya wafungwa wa kisiasa, ikiwemo kukamatwa isivyo halali, kupigwa, ubakaji na hata mauaji. Mwanasheria huyo aliyaelezea matukio ya uhalifu, upendeleo na rushwa, ikiwemo uporaji katika kampuni kubwa ya kijeshi ya utengenezaji chuma na uhandisi ya METEC, inayozalisha vifaa vya kijeshi na bidhaa nyingine za kiraia.
"Mikataba ilifanyika kupitia mitandao ya familia na washirika. Matokeo yake, nchi imepata hasara kubwa", alisema Tsegaye.
Siku ya Jumanne mkuu zamani wa kampuni hiyo ya kijeshi Kinfe Dagnew ambaye ni meja Jenerali katika jeshi la Ethiopia amekamatwa karibu na mji wa Kaskazini magharibi wa Humera, ulio karibu na mpaka wa Sudan na Eritrea.
Kwa mujibu wa mwanasheria mkuu, uchunguzi uliofanywa umebaini kwamba kampuni hiyo ilifanya manunuzi ya kimataifa yanayofikia Dola bilioni 2 bila kufuata michakato ya zabuni.
Kwa miongo kadhaa kampuni hiyo ya METEC imekuwa kiungo muhimu katika uchumi uliodhibitiwa na taifa na jeshi. Maafisa wa juu wa kampuni hiyo inayotengeneza vifaa vya kijeshi na kujihusisha na sekta nyinginezo kama vile kilimo na ujenzi wengi ni maafisa jeshi.
Kukamatwa huko kwa maafisa ni hatua mojawapo ya waziri mkuu mpya Abiy aliyeingia madarakani baada ya mtangulizi wake kun'gatuka katikati mwa maandamano makubwa ya kuipinga serikali. Abiy anaonekana kuwa na dhamira ya kuleta mageuzi na demokrasia nchini humo.
Hadi sasa amewaachia huru wafungwa wengi wa kisiasa na kuyaondolea marufuku makundi ya upinzani ambayo wakati mmoja yalitangazwa kuwa mashirika ya kigaidi.
Waziri huyo mkuu pia ameweza kurejesha upya mahusiano ya kidiplomasia na hasimu wake wa muda mrefu Eritrea mapema mwaka huu na kukomesha rasmi vita ya mpaka ambayo iliwaua makumi kwa maelfu ya raia kati ya mwaka 1998-2000.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga