1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maadhimisho ya miaka 80 tangu kuanza Vita Vikuu vya pili

Daniel Gakuba
31 Agosti 2019

Jumapili ya Septemba 1 zinafanyika kumbukumbu za miaka 80 tangu kuanza kwa vita vikuu vya pili. Kumbukumbu hizo zinafanyika katika mji wa Wielun nchini Poland, zikihudhuriwa na viongozi wengi muhimu wa nchi za Magharibi.

https://p.dw.com/p/3OnxV
29.07.2014 DW Feature Foto Dokumentation Doku Zerstörtes Haus, Wielun
Picha: DW

Miaka 80 imetimia tangu kuanza kwa mashambulizi ya jeshi la Ujerumani iliyotawaliwa na Wanazi dhidi ya Poland, ambayo yalikuwa mwanzo wa Vita Vikuu vya Pili. Rais wa shirikisho la Ujerumani Frank Walter Steinmeier na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, wanashiriki katika kumbukumbu zinazofanyika nchini Poland, kuvikumbuka vita hivyo na wanga wake.

Jan Tyszler anakumbuka kilichotokea alfajiri ya Septemba mosi mwaka 1939, katika makazi ya familia yake kwenye mji wa Wielun nchini Poland, umbali wa km 200 kutoka kwenye mpaka kati ya nchi hiyo na Ujerumani. Anasema mlio wa ving'ora vya tahadhari ulimkurupusha usingizini, na alipoamka aliwakuta wazazi wake kwenye veranda, wakishangaa kilichotokea. Wao walidhani ving'ora hivyo vilikuwa vya majaribio tu.

Kutanda kwa wingu la vita

Tyszler ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka sita, anasema tangu Agosti mwaka huo harufu ya vita ilikuwa kila mahali, ila hakuna aliyedhani kuwa mji mdogo wa Wielun ambao haukuwa na chochote cha maana ungekuwa mahali pa kuanzia vita hivyo. Mji wao ulikuwa na ulinzi wa wanajeshi wachache tu.

Fokus Europa  Polen Wielun
Ndege za kivita za Wanazi ziliwauwa raia wengi mnamo vita vikuu vya piliPicha: DW

Haraka haraka Jan Tyszler na familia yake walijificha katika handaki lililokuwa chini ya karakana ya baba yake, na anakumbuka kuwa ilipofika jioni, nyumba yao pekee ndio ilikuwa bado imesimama katika mtaa mzima. Kama wakazi wengine mia kadhaa walioishi mjini Wielun, familia yao iliuhama mji huo, na walipoingia wanajeshi wa wanazi, mji ulikuwa mtupu.

Mashambulizi ya anga ya majeshi ya wanazi yaliongozwa na Wolfram von Richthofen, ambaye Aprili mwaka 1937 alishiriki katika kuuangamiza mji wa  Geurnica Kaskazini Mashariki mwa Uhispania na kuangamiza maisha ya maelfu ya wakazi wake. Katika mbinu hiyo mpya ya mashambulizi ya anga, mauaji ya raia yalichukuliwa kama kitu kinachokubalika, na von Richthofen alitaka kuujaribu uzoefu wa Geurnica nchini Poland.

Mhanga wa uhalifu wa kivita

Wielun ulikuwa mji wa kwanza kushuhudia uhalifu wa kivita katika Vita Vikuu vya Pili. Asilimia 70 ya majengo yake yaliharibiwa, na kati ya watu 1600 walioishi katika mji huo mdogo, 1200 waliuawa.

Polen, Wieluń - Jan und Schwester Maria 1937
Pichani kulia ni Jan Tyszler akiwa na dada yake Maria wakati wa vita vikuu vya piliPicha: privat

Mashambulizi katika mji huo yalitanguliwa na visa kadhaa vya uchokozi, ambavyo vilitumiwa na kiongozi wa utawala wa kinazi Adolf Hitler kuionyesha Ujerumani kama upande uliokuwa ukifanyiwa uonevu. Vyombo vya habari vya Ujerumani vilichapisha ripoti zilizowatuhumu Wapoland wanaoishi kwenye ardhi ya Ujerumani, kula njama ya uasi wakisaidiwa na jeshi la Poland.

Dakika 10 tu baada ya mashambulizi dhidi ya mji wa Wielun, ilikuwa zamu ya bandari ya Westerpalatte katika mji wa Gdansk, ambayo licha ya kuwa wakazi wengi walikuwa Wajerumani, na wenye hadhi ya mji huru kwa mujibu wa mkataba wa Versailles, ulikuwa chini ya mamlaka ya Poland.

Nembo ya ushujaa nchini Poland

Katika vita hivyo waliuawa Wajerumani 3,400 na huku upande wa Poland ukipoteza watu 15. Hadi leo, mapigano hayo ya Westerplatte yanachukuliwa kama nembo ya ushujaa wa wanajeshi wa nchi hiyo, dhidi ya jeshi la wanazi ambalo lilikuwa na nguvu kubwa kupindukia.

Katika kumbukumbu za miaka 70 tangu kuanza kwa Vita Vikuu vya Pili, Rais wa Urusi Vladimir Putin na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel walijiunga na rais wa Poland wakati huo Lech Kaczynski mjini Gdansk, na Kaczynski alikemea mbele ya Putin uvamizi wa jeshi la Urusi nchini Georgia, akiuita mienendo mipya ya kifashisti.

Kwamba kumbukumbu za mwaka huu hazifanyiki Gdansk, bali Wielun ambako pia rais wa shirikisho la Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ni mgeni mwalikwa sio tukio la kushtukiza, ila ni katika juhudi za serikali ya sasa inayoongozwa na chama cha Sheria na Haki, PiS chenye sera za mrengo mkali wa kizalendo, kuchochea hisia za uzalendo kupitia kumbukumbu za historia.

Monika Sieradzka/DW