Maadhimisho ya kupigania haki za raia weusi Marekani
8 Machi 2015Obama ambae ni Rais wa kwanza mweusi nchini Marekani aliyatamka hayo katika maadhimisho ya mwaka wa 50 tokea polisi wa Marekani walipowashambulia kikatili hasa Wamarekani weusi waliokuwa wanafanya maandamano ya amani kwenye mji wa Selma katika jimbo la Alabama.
Polisi walifanya ukatili
Polisi walitumia virungu na mabomu ya kutoa machozi kuyazuia maandamano hayo. Katika hotuba yake Rais Obama aliwapongeza wanaharakati waliojitoa mhanga, miaka 50 iliyopita, kufanya maandamano ili watu weusi wapate haki zao. Amesema maandamano hayo ndiyo yaliyomfungulia njia ya kuingia Ikulu ya Marekani.
Licha ya kupigwa virungu walisonga mbele
Obama aliwaambia watu waliohudhuria maadhimisho ya mjini Selma kwamba, wamekwenda kuuenzi ujasiri wa Wamarekani wa kawaida, waliokuwa tayari kupigwa virungu,mabomu ya machozi, na kukanyagwa na farasi; na licha ya kuvunjwa mbavu, wanawake na wanaume hao walisonga mbele na maandamano. Obama amesema wanaharakati hao walisimama imara kama nyota ya kaskazi.
Rais Lyndon Johnson apitisha sheria
Kutokana na harakati hizo na zingine, Rais wa Marekani wa wakati huo Lyndon Johnson aliipitisha sheria ya kuwapa haki watu weusi ya kupiga kura.
Hata hivyo Rais Obama ameeleza kuwa sheria hiyo imo hatarini kwa mara nyingine, kwa sababu serikali inataka kuzikaza sukurubu za utaratibu wa kuwaandikisha wapiga kura. Obama aliuliza kwa nini sheria hiyo ihatarishwe, huku akitilia maanani kwamba, sheria hiyo ilitiwa nguvu upya na marais wa Republican, Ronald Reagan na George W Bush aliehudhuria madhimisho ya mjini Selma.
Rais Obama amewataka wabunge 100 waliohudhuria maadhimisho ya mjini Selma wajiunge na wabunge wengine ili wailinde sheria inayowapa Wamarekeni wote haki ya kupiga kura. Katika hotuba yake Obama pia aligusia juu ya matukio ya hivi karibuni yaliyohusu kuuliwa Wamarekani weusi na polisi nchini Marekani.
Ubaguzi wa rangi bado upo
Matukio hayo yalisababisha maandamano na malamiko juu ya kuwepo rasmi kwa ubaguzi wa rangi wa kina kirefu.Obama ameeleza kuwa watu wanahitaji kuyafungua macho na nyoyo zao ili kujua kwamba historia ndefu ya ubaguzi bado inalipelemba taifa la Marekani. Amesema "tunajua kwamba safari yetu bado haijafikia mwisho" Ameeleza kuwa ushindi kamili dhidi ya ubaguzi bado haujapatikana.
Rais Obama pia alitilia maanani kwamba wabunge mia moja walikuwapo kwenye maadhimisho ili kuwaenzi wanaharakati waliokuwa tayari kufa ili kuilinda sheria ya kuwapa watu wote haki ya kupiga kura.
Mwandishi:Mtullya Abdu.afpe/rtre.
Mhariri: Bruce Amani