M23 wakiteka tena kijiji cha Kishishe mashariki mwa Kongo
15 Novemba 2023Kundi la waasi la M23 limekiteka tena kijiji cha Kishishe mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Waasi hao walijiondoa katika kijiji hicho mwanzoni mwa mwezi Aprili, sambamba na maeneo mengine katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Duru zinasema Kijiji hicho kimekimbiwa kwa kiasi kikubwa na wakaazi wake, lakini mapigano yameendelea kwa siku mbili, kabla ya jeshi kuingilia kati.
Soma kuhusu: Jeshi la Congo lawazuia waasi wa M23 kuingia Goma
Mwakilishi mmoja wa asasi ya kiraia katika eneo hilo amethibitisha taarifa za M23 kukidhibiti Kijiji cha Kishishe tangu Jumatatu, taarifa zilizothibitishwa na vyanzo vingine viwili vya usalama.
Umoja wa Mataifa ulisema katika ripoti yake kwamba waasi wa M23 waliwaua watu 171 katika kijiji cha Kishishe Novemba mwaka uliopita, shutuma ambazo M23 imezikanusha.