1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LUXEMBOURG: Umoja wa Ulaya wajiandaa kupeleka misaada kwa Wapalestina

18 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBqY

Umoja wa Ulaya umesema unajiandaa kupeleka misaada kwa Wapalestina kufuatia kuundwa kwa serikali mpya ya mpito ya Palestina ambayo haijumlishi wabunge wa chama cha Hamas.

Mratibu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, ameuambia mkutano wa mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Umoja wa Ulaya mjini Luxembourg kwamba umoja huo unatakiwa kutafuta njia za kuwapelekea misaada Wapalestina walio katika Ukanda wa Gaza.

Hata hivyo amesema sharti kutafutwe njia ambayo haitaruhusu misaada kuwafikia wanachama wa chama cha Hamas, kilichonyakua madaraka katika eneo la Ukanda wa Gaza wiki iliyopita.

´Tutashirikiana na serikali hii. Tutatoa fedha ambazo tumekuwa tukizizuilia kwa sababu hatukataka zichukuliwe na Hamas na zitumike katika vitendo vya ugaidi. Kuhusiana na Gaza tunawajibu wa kuwasaidia Wapalestina. Hatuwezi kuwaacha peke yao Wapalestina wanaoishi Gaza. Tumemwambia waziri mkuu mpya na yeye amejitolea kwa dhati.´

Umoja wa Ulaya ulisitisha misaada kwa Wapalestina mnamo mwezi Machi mwaka jana wakati serikali iliyoongozwa na chama cha Hamas ilipochukua madaraka katika maeneo ya Wapalestina.

Sambamba na taarifa hiyo, shirika linalowahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa limeanzisha shughuli zake za kutoa huduma kwa wakimbizi wa kipalestina katika Ukanda wa Gaza hii leo.

Shirika hilo limeanza tena kutoa huduma katika eneo hilo baada ya kusitisha kazi yake kwa siku tano kufutia kuuwawa kwa wafanyakazi wake wawili wakati wa machafuko baina ya makundi hasimu ya Fatah na Hamas.