1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Luis Enrique: Sipendi mechi bila mashabiki

21 Mei 2020

Kocha wa Uhispania Luis Enrique amesema hapendelei mechi kuchezwa bila mashabiki uwanjani. Kauli yake inakuja huku ligi zikiwa zinaanza kuchezwa tena ingawa katika viwanja vitupu baada ya kutatizwa na virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3caMQ
FC Barcelona Luis Enrique
Picha: Getty Images/D. Ramos

"Kucheza mechi bila ya mashabiki inahuzunisha zaidi ya huzuni unayopata unapocheza muziki na dadako," alisema Luis Enrique.

Jumamosi Mei 16 Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga ilikuwa ligi ya kwanza kuu kuanza tena kucheza mechi zake na wachezaji walikuwa hawasherehekei magoli pamoja ili kupunguza uwezekano wa kuambukizana virusi vya corona na viwanja ambavyo kawaida huwa vimsheheni mashabiki, vilikuwa vitupu.

"Inatisha sana, nilitazama Bundesliga na ilikuwa inasikitisha. Unaweza kusikia wanayosema wachezaji na hili linapoteza ule utamu," alisema Enrique ambaye ni kocha wa zamani ambaye pia alikuwa mchezaji wa Barcelona.

Lakini kocha huyo vile vile amekiri kwamba kuwepo kwa michezo inayoonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni ni jambo ambalo litakuwa kama afueni kwa mamilioni ya watu ambao wamefungiwa majumbani na amri za serikali zao ili kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.