Luis Enrique atangaza kikosi cha Uhispania
31 Agosti 2018Enrique amewaita wachezaji 24 kwa ajili ya michezo ya timu hiyo dhidi ya England na Croatia katika ligi ya mataifa.
Kocha huyo wa zamani wa Barcelona amewajumuisha wachezaji 13 kutoka kikosi kilichocheza katika kombe la dunia, ikiwa ni pamoja na David de Gea, Sergio Ramos, Sergio Busquets na Diego Costa.
Miongoni mwa wale wanaorejea katika kikosi hicho baada ya kukosa nafasi katika kikosi kilichokwenda katika kombe la dunia ni pamoja na Alvaro Morata na Sergio Roberto.
Andres Iniesta , Gerard Pique na David Silva tayari walitangaza kujiuzulu kutoka timu hiyo ya taifa kufuatia kuondolewa kwa Uhispania na wenyeji wa mashindano hayo Urusi katika duru ya timu 16.
Kocha wa mpito Fernando Hierro alikuwa akikifundisha kikosi cha Uhispania katika kombe la dunia kwasababu Julen Lopetegui alifukuzwa siku mbili kabla ya kuanza kwa mashindano hayo ya kombe la dunia kwa kukubali kazi ya kuifunza Real Madrid bila ya kuwaambia maafisa wa shirikisho la kandanda la Uhispania.
Enrique hakuzungumzia juu ya wachezaji aliowaacha na kusema "mshangao zaidi" unatarajiwa hapo baadaye.
Kocha huyo amemjumuisha katika kikosi chake mlinzi Diego Lllorente licha ya kuwa hataweza kucheza kutokana na kufanyiwa upasuaji katika mguu wake wa kushoto uliovunjika.
Enrique amesema mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 25 anaonekana kuwa mchezaji mzuri sana hapo baadaye na anataka kupata uzoefu wa kuwa pamoja na wachezaji wengine katika timu ya taifa. Uhispania inacheza na England Septemba 8 na wenyeji Croatia siku tatu baadaye.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Iddi Ssessanga