Luanda. Wakaazi wa Uige nchini Angola wawapiga mawe wafanyakazi wa shirika la afya duniani WHO kwa kuhofu kuwa wanasambaza virusi vya ugonjwa wa Marburg.
10 Aprili 2005Wafanyakazi wa shirika la afya duniani WHO wanaopambana na virusi vya ugonjwa wa Marburg nchini Angola wamelazimika kusitisha kazi hiyo katika eneo moja baada ya wakaazi wa eneo hilo wenye hofu kuyarushia mawe magari ya shirika hilo. Maafisa wamesema jana kuwa WHO ilisitisha kazi zake katika baadhi ya sehemu za wilaya ya Uige kaskazini magharibi ya Angola siku ya Ijumaa kufuatia shambulio hilo lililofanyika Alhamis. Wakaazi hao wakihofia kuwa waganga wa shirika hilo huenda ndio wanasambaza virusi hivyo ambavyo vimesababisha watu 184 kupoteza maisha yao, baadhi yao wafanyakazi wa idara ya afya.
WHO hata hivyo imesema jana kuwa imeanza tena kampeni ya kupambana na virusi hivyo katika jimbo la Uige, ambako ndiko kulikoathirika zaidi.
Idara ya afya nchini Angola, ikitoa idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa huo wa Marburg, imesema , watu jumla ya watu 213 wamefariki, ikiwa ni idadi kubwa kabisa kuwahi kutokea tangu kuzuka kwa ugonjwa huo.