LUANDA : Mlipuko wa Marbug ni mbaya sana kuliko Ebola
9 Aprili 2005Mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marbug nchini Angola ni mbaya sana uliko hata Ebola.
Kauli hiyo imetolewa na mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa ugonjwa huo hapo jana wakati chombo hicho cha dunia kikizinduwa wito wa dharura kwa ajili ya kupatiwa michango ya kupambana na homa ya ugonjwa huo ambao umegharimu maisha ya watu 180.
Allrangara Yokouibd kutoka Shirika la Afya Duniani la Umoja wa Mataifa amekaririwa akisema homa inayovujisha damu ya Marburg ni mbaya sana kuliko hata ile ya Ebola.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Luanda amesema wamekuwa na magonjwa kadhaa ya Ebola katika eneo hilo lakini hayakuwahi kusababisha kiwango kikubwa cha vifo kiasi hicho.
Mjini Geneva Shirika la Afya Duniani limesema mripuko wa ugonjwa huo mbaya kabisa kuwahi kutokea duniani bado haukudhibitiwa.