1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lori la gesi lasababisha ajali na kuua watu 30 Naivasha

Oumilkheir Hamidou
11 Desemba 2016

Zaidi ya watu 30 wameteketea kwa moto hadi kufa wakiwemo maafisa 11 wa polisi. Ni baada ya lori lililosheheni gesi kuyagonga magari mengine na kulipuka nje ya mji wa Naivasha. Inahofiwa huenda idadi ya vifo itaongezeka.

https://p.dw.com/p/2U68X
Kenia Explosion von einem Tanklastwagen
Picha: Reuters/T. Mukoya

Zaidi ya watu 30 wameteketea kwa moto nchini Kenya, baada ya lori lililobeba gesi kuyagonga magari mengine na kulipuka katika barabara kuu kilomita chache nje ya mji wa Naivasha. Kwa mujibu wa maafisa, mkasa huo ulifanyika usiku wa kuamkia Jumapili.

Pius Masai ambaye ni afisa wa kitengo cha kitaifa kinachoshughulikia majanga nchini Kenya amesema kufikia mwendo wa saa kumi na moja alfajiri, waliokufa walifikia 33.  Ameongeza kuwa jumla ya magari 11 yaliteketea kwa moto. Waokozi wanaendelea kupekua eneo la ajali kubaini kama kuna miili zaidi.

Gazeti la Sunday Standard, limesema idadi ya waliokufa inaaminika kuongezeka na kufikia watu 40. Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limesema dereva wa lori hilo, alishindwa kulidhibiti lilipokosa mwelekeo kabla ya kuyagonga magari mengine barabarani kisha likalipuka na kushika moto.  Moto huo ukasambaa kwa kasi hadi kushika magari mengine.

Gari la abiria, pamoja na lori la polisi ni miongoni mwa magari yaliyoteketea kwa moto. Maafisa 11 wa polisi wa kupambana na ghasia ni kati ya wale ambao wamefariki kwenye mkasa huo.

Gari la polisi likiteketezwa na moto
Gari la polisi likiteketezwa na motoPicha: Reuters/T. Mukoya

Rais Uhuru Kenyatta amehimiza uchunguzi kamili ufanywe

Rais wa Kenya uhuru Kenyatta kupitia taarifa kwa vyombo vya habari ametaka uchunguzi kamili kufanywa dhidi ya kile anachosema ni ukiukwaji wa sheria inayopiga marufuku malori yanayobeba bidhaa hatari au shehena nyingi kusafiri usiku na katika baadhi ya barabara. Amesema lori lililosababisha ajali hiyo ya kusikitisha halikupaswa kuwa katika barabara hiyo wakati huo wa mkasa.

Kulingana na polisi, lori hilo lililokuwa na nambari za usajili za Uganda, lilikuwa likisafiri kwa mwendo wa kasi na lilikosa mwelekeo  pale lilipopita matuta ya barabarani kwa mwendo huo.

Zaidi ya watu 50 waliojeruhiwa kufuatia mkasa huo wamefikishwa katika hospitali ya kibinafsi mjini Naivasha. Walioshuhudia wameelezea kuona moto mkubwa ukiteketeza magari yaliyokuwa na abiria au madereva ndani. Shughuli za kuondoa miili iliyoteketea kupindukia ilianza punde baada ya wazima moto kufaulu kuuzima moto huo.

George Rono aliyekuwa akiliendesha gari lake anasema aliponea chupuchupu kwa kuliendessha gari lake nje ya barabara punde aliposikia magari yakipiga honi na kufuatwa na mlipuko ulioambatana na moto mkubwa. ‘‘Ni kama filamu ya kutisha. Itanitatiza akili kwa muda mrefu. Wewe fikiria moto huo mkubwa watu wakiteketea ndani yake. Na sasa nimeona wengine wameketi ndani ya magari hayo lakini wameteketea‘‘. Amesema Jane Muthoni ambaye ni muuzaji katika duka karibu na eneo la mkasa.

Gari lililoteketea kwa moto
Gari lililoteketea kwa motoPicha: Reuters/Stringer

Kutokana na kiwango cha athari za ajali hiyo, inahofiwa huenda idadi ya vifo ikaongezeka.

Ajali hiyo inajiri wakati Kenya inakumb wa na mgomo wa madakitari na wauguzi katika hospitali za serikali.

Barabara hiyo kuu ambayo huwa na shughuli nyingi imekuwa na visa vingi vya ajali. Mwaka 2009, zaidi ya watu 100 walifariki na 200 kujeruhiwa baada ya lori la mafuta kubingiria na kuwaka moto pale  wakaazi wa karibu walilikimbilia kuchota mafuta.

Mwandishi: Juma John /AFPE/APE

Mhariri: Hamidou Oumilkheir