1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON:Suala la Waasi wa PKK laendelea kuzusha mjadala

23 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7DE

Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown amefanya mazungumzo na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan juu ya hali katika eneo la kaskazini mwa Iraq.

Katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kukutana na Erdogan, Gordon Brown amelaani ghasia za kigaidi za mwishoni mwa juma zilizofanywa na waasi wa PKK ambapo wanajeshi 12 wa Uturuki waliuwawa.

Kwa upande wake Erdogan amesema nchi yake haitasubiri muda mrefu kwa iraq kuchukua hatua dhidi ya waasi hao.Ameongeza kusema wanajeshi wa Uturuki wataingia kaskazini mwa Iraq wakati wowote kuwasaka waasi hao na pia watafikiria kuweka vikwazo vya kibiashara dhidi ya Iraq.Lakini pia amekumbusha.

Oktoba 17 bunge la Uturuki lilipitisha muswaada wa sheria unaotaka pafanyike opresheni za kijeshi dhidi ya ugaidi kaskazini mwa Iraq.Mimi nasisitiza kwamba opresheni kama hiyo itawalenga tu waasi wa PKK kwa sababu sisi wakati wote tumekuwa tukishirikiana na wairaq ambao katika Historia wanakabiliana na hali ngumu.Sisi hatuna malengo ya kutaka maslahi yoyote Iraq na wala juu ya Umoja wa Kisiasa nchini humo bali ni kinyume chake.

Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Ali Babacan pia amekutana na uongozi wa juu wa Iraq na kujadili suala la waasi wa kikurdi wa PKK.

Babacan amesema Uturuki inataka kufuata hatua zote za kidiplomasia na kisiasa na serikali ya mjini Baghdad kabla ya kuchukua uamuzi wa kijeshi dhidi ya waasi hao.