LONDON : Repoti yaonya juu ya mabadiliko ya hali ya hewa
31 Oktoba 2006Repoti ya serikali ya Uingereza imeonya kwamba kuongezeka kwa kiwango cha ujoto duniani kunatishia kuwapotezea makaazi mamilioni ya watu na kuharibu uchumi wa dunia.
Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair amezinduwa repoti hiyo ya kurasa 580 ya uchambuzi wa Nicholas Stern mchumi mkuu wa zamani wa Benki ya Dunia ambayo imedokeza kwamba kutochukuliwa kwa hatua ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kunaweza kugharimu kati ya asilimia 5 na 20 ya pato la jumla la ndani ya nchi kwa mwaka.
Blair amesema kwamba hivi sasa wanajuwa kuwa hatua za dharura zitazuwiya maafa na kuwekeza hivi sasa katika kuzuwiya mabadiliko hayo ya tabia nchi kutaleta faida kubwa sana baadae.
Kamati ya mabadiliko ya hali ya hewa au tabia nchi ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake mjini Bonn Ujerumani inasema utowaji wa gesi zenye kuathiri mazingira katika mataifa yenye maendeleo ya viwanda umeongezeka kwa asilimia 2.4 kati ya mwaka 2000 na 2004 hususan kutokana na kufufuka kwa uchumi katika nchi za zamani za kikoministi Ulaya ya mashariki.
Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kyoto unataka kupunguzwa kwa asilimia 5 gesi zenye kuathiri mazingira ifikapo mwaka 2012.