London. Makubaliano ya bajeti ya Ulaya ni vigumu kufikiwa akiri Blair.
28 Oktoba 2005Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair amekiri kuwa makubaliano ya bajeti ya umoja wa Ulaya yatakuwa vigumu kufikiwa , lakini ameongeza kuwa ni muhimu kwa ajili ya kundi hilo la mataifa.
Blair alikuwa akizungumza kufuatia mkutano usio rasmi wa umoja wa Ulaya nje kidogo ya mji wa London.
Viongozi hao 25 wa serikali pia wameshindwa kupata muafaka juu kuboresha sera za kiuchumi na kijamii katika umoja huo.
Kiongozi wa tume ya Ulaya Jose Manuel Barroso wakati huo huo ameeleza matarajio yake kwa tahadhari katika kupatikana kwa makubaliano ya bajeti katika mkutano wa umoja wa Ulaya mwezi Desemba. Duru ya mwanzo ya mazungumzo ilivunjika mwezi wa Juni huku kukiwa na mzozo juu ya fedha inazorejeshewa Uingereza pamoja na ruzuku za kilimo.