LONDON. Chama cha Labour chashinda uchaguzi nchini Uingereza.
6 Mei 2005Waingereza wamemchagua tena shingo upande bwana Tony Blair kuwa waziri mkuu mpya kuliongoza taifa hilo kwa awamu ya tatu.
Blair amesema ijapo raia wanataka chama cha Labour kiendelee kuiongoza Uingereza, ni jambo lililo wazi kwamba wanataka kuyapunguza mamlaka yake, kwani idadi ya wabunge wa chama chake safari hii itakuwa ndogo.
Imebashiriwa kwamba chama cha Labour huenda kipate viti 80 kati ya viti 656 bungeni. Blair ameshinda tena katika sehemu ya uwakilishi bungeni ya Segdefield, licha ya changamoto aliyoipata kutoka kwa Reg Keys, ambaye mwanawe aliyekuwa mwanajeshi, alifariki dunia nchini Irak. Katika hotuba yake ya shukurani, Blair amesema swala la Irak limeigawa nchi hiyo lakini sasa waingereza wote wanaweza kuungana tena pamoja.
Blair amesema awamu hii ndiyo itakayokuwa ya mwisho, hali ambayo huenda imfanye asiweze kuwa na usemi mkubwa huku wabunge wa chama chake wakipigania nafasi ya kutaka kumrithi. Kumekuwa na tetesi kwamba Blair huenda ajiuzulu kabla awamu yake kumalizika na kumuachia wadhifa wake waziri wa fedha bwana Gordon Brown, ambaye amechaguliwa tena kuwa mbunge.
David Blunkett na waziri wa mambo ya kigeni, bwana Jack Straw, wameshinda tena katika maeneo yao ya uwakilishi bungeni.
Chama cha kikonsavativ cha Michael Hawad, kilichoongozwa zamani na Margaret Thatcher na Winston Churchill, kinaelekea kitakuwa upande wa upinzani kwa mara nyengine ya tatu. Hata hivyo kimejipatia ushindi katika maeneo muhimu nchini humo.
Chama cha Liberal Democrats kimejikakamua vilivyo lakini hakijaweza kufua dafu.