1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Loew azungumzia nafasi za timu ya Ujerumani

11 Juni 2018

Zimebaki siku tatu tu kabla ya kuanza tamasha kubwa kabisa la kandanda duniani. Kombe la Dunia la FIFA 2018 linaanza Urusi Alhamisi tarehe 14. Tayari timu zinaendelea kuwasili Urusi na kuanza kijifahamisha na mazingira

https://p.dw.com/p/2zIvU
Fußball Länderspiel Deutschland - Saudi-Arabien Joachim Löw
Picha: picture-alliance/dpa/GES/M. I. Guengoer

Ujerumani wanawasili kesho Jumatano wakiwa mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia lakini kocha Joachim Loew amesisitiza kuwa wachezaji wake lazima waondoe makosa madogo madogo na kila kitu kiwe sawa ili waweze kuhifadhi kombe hilo.

Loew anasema wapinzani wamejipanga sawa sawa kwa hiyo  vijana wake wanapaswa kuwa makini sana katika kila mechi, lazima wawe macho kuanzia mwanzo na kucheza hadi upeo wao wa juu.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 58 anasema Kama Ujerumani watakuwa timu ya kwanza tangu Brazil, katika mwaka wa 1958 na 1962, kuhifadhi Kombe la Dunia, basi kila kitu lazima kiwe sawa tu.

Ushindi wa karibuni wa 2-1 dhidi ya Saudi Arabia ulikuwa wao wa kwanza katika mechi sita na Loew anasema ulikuwa mtihani mzuri kwao. Tulipoteza nafasi nyingi sana na tukamruhusu mpinzani kupata fursa nyingi. Naamini kipindi cha kwanza kilikuwa kizuri. Mchezo wetu ulikuwa mwepesi kutokana na nafasi nzuri tulizopata. Katika kipindi cha pili tukapunguza kasi. Katika ulinzi tunapaswa kuimarika na sio kuwacha mianya mingi.

Mkataba wa Loew ulirefushwa karibuni hadi mwaka wa 2022, wakati wa Kombe la Dunia nchini Qatar na uungaji mkono anaopata kutoka kwa shirikisho la kandanda la Ujerumani – DFB una maana hana shinikizo lolote la kutoka nje

Fussball Herren Saison 2017 18 Länderspiel in Leverkusen Deutschland Saudi Arabien Marco Reus
Ujerumani ni moja ya timu zinazopigiwa upatuPicha: Imago/M. Koch

Usalama waimarishwa

Wahuni, wadukuzi wa mitandao na unaguzi: hayo ndo mambo ambayo yamegonga vichwa vya habari kabla ya kuanza dimba la Kombe la Dunia la 2018. Maafisa wa Urusi hata hivyo, wanasema mashabiki wanapaswa kujihisi  kuwa salama maana watakaribishwa vizuri nchini humo. Kwa Urusi, kombe la dunia 2018 ni nafasi ya kuuonyesha uso wa kirafiki kwa ulimwengu kama anavyoeleza Rais Vladmir Putin

Nnawakaribisha mashabiki wa kandana na timu bora za kandanda duniani, wale wote ambao tayari wamefika URUSi, na wale ambao wanajiandaa kushiriki katika tamasha kubwa la kimataifa Kombe la Dunia la FIFA. Kwa nchi yetu ni furaha kubwa na heshima kuwapokea wawakilishi kutoka kwa familia kubwa ya kandanda.

Miongoni mwa hatua za usalama zilizochukuliwa ni pamoja na marufuku ya kuuza silaha na kemikali hatari lakini pia uuzaji na unywaji wa pombe.

Russland Moskau - FIFA Fußball WM-Auslosung in Russland
Rais Putin anasema mashabiki wanakaribishwa UrusiPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Kwa kipindi cha miezi miwili, maandamano yote na matukio ya umma katika miji inayoandaa mechi za Kombe la Dunia ambayo hayahusiani na kandanda lazima yapewe kibali cha maafisa wa miji, polisi lakini pia kutoka kwa idara ya ujasusi.

Mji wa Volgograd ni miongoni mwa miji itakayotumika kwa Kombe la Dunia na meya wake Andrei Kosolapov anaapa kuwa sasa uko salama kikamilifu. "urusi ni moja ya nchi ambazo zitapambana na ugaidi katika kila njia. Hakika, tulikuwa na matukio kadhaa mabaya katika mwaka wa 2013.  Tumerekebisha kazi yetu. Vikosi vya usalama na raia wa Volgograd kila maa huwa makini kwa vitisho. Hivyo nadhani maovu kama hayo hayatatokea tena.

Wizara ya ulinzi ya Urusi na idara ya usalama wa taifa, zimeweka mitambo ya kisasa ya ulinzi wa angani katika miji 11, ikiwa ni pamoja na baadhi ya mifumo iliyotumika kukilinda kituo cha jeshi la angani nchini Syria dhidi ya mashambulizi ya ndege zisizoruka na rubani

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman