1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoArgentina

Messi ashinda tuzo ya nane ya Ballon d'Or

31 Oktoba 2023

Nahodha wa timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi ameweka rekodi kwa kushinda tuzo ya nane ya Ballon d'Or ya mchezaji bora wa mwaka duniani.

https://p.dw.com/p/4YDU2
Frankreich | 2023 Ballon d'Or in Paris | Lionel Messi
Mchezaji Lionel MessiPicha: Pascal Le Segretain/Getty Images

Messi amewapiku mchezaji bora wa mwaka wa shirika la kandanda Ulaya -UEFA Mnorway Erling Halaand wa Manchester City, na mshambuliaji wa Paris Saint Germain Kylian Mbappe.

Messi anayechezea Inter Miami, na ambaye alishinda tuzo hiyo mara ya mwisho mwaka wa 2021, alikuwa na mchango muhimu katika kuiongoza Argentina kushinda taji lao la kwanza la Kombe la Dunia katika miaka 36 wakati walipowachabanga mabingwa watetezi Ufaransa.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 sasa anamzidi mpinzani wake Cristiano Ronaldo na tofauti ya mataji matatu ya Ballon d'Or. Ronaldo alishinda tuzo yake ya mwisho kati ya tano katika mwaka wa 2017. Messi sasa amemaliza miongoni mwa walioshika nafasi tatu bora mara 14 kwa jumla ikiwa ni rekodi mpya, huku akimaliza katika nafasi ya pili mara tano.

Frankreich | 2023 Ballon d'Or in Paris | Lionel Messi
Lionel Messi akipokea tuzo ya Ballon d´Or: Paris Ufaransa:30.10.2023Picha: Michel Euler/AP/picture alliance

"Sikuweza kufikiria kuwa na taaluma kama niliyokuwa nayo. Kila kitu ambacho nimefanikiwa. Nna bahati nimekuwa nikiichezea timu bora duniani, timu bora katika historia. Inapendeza kushinda mataji haya ya kibinafsi. Kushinda Copa America na kisha Kombe la Dunia, kufanikiwa hilo inapendeza." Alisema Messi.

Alipoulizwa kama ataendelea kucheza kandanda hadi Kombe la Dunia la 2026, Messi alisema: "Sifikirii kuhusu hilo. Ntafurahia taaluma yangu siku baada ya siku. Kwanza kutakuwa na Copa America nchini Marekani mwaka wa 2014 kisha Kombe la Dunia. Sifikirii kuhusu hilo."

Messi alinufaika na mabadiliko ya karibuni ya vigezo vya wawaniaji ambapo tuzo hiyo inazingatia rekodi ya mchezaji kwa msimu uliopita, badala ya kalenda nzima ya mashindano. Muargentina huyo alishinda licha ya kuwa na msimu wa mwisho usioridhisha katika klabu ya PSG, hata kama alikuwa mshindi wa taji la Ligue 1.

Mbappe alikuwa mchezaji nyota katika timu hiyo, akifunga magoli 41, na pia alikuwa mfungaji bora katika Kombe la Dunia na mabao nane, ikiwemo hattrick katika fainali ambayo Ufaransa ilishindwa na Argentina kupitia mikwaju ya penalti.

Frankreich | 2023 Ballon d'Or in Paris | Erling Haaland
Mchezaji Erling HaalandPicha: Stephanie Lecocq/REUTERS

Haaland, mwenye umri wa miaka 23, alikuwa mmoja wa wachezaji waliopigiwa upatu kubeba taji lake la kwanza la Ballon d'Or baada ya kufunga mabao 52 katika mechi 53 katika mashindano yote msimu uliopita wakati City ilishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi ya Premier na Kombe la FA.

Lakini mafanikio ya Messi katika Kombe la Dunia Qatar , ambapo alipata tuzo ya mpira wa dhahabu ya mchezaji bora wa mashindano hayo na njumu ya fedha kwa kufunga mabao sab ana asisti tatu, vilimsaidia kumpiku Mmnorway huyo katika tuzo ya Ballon d'Or.

Itabakia kuona kama Messi atashiriki kwa mara nyingine katika kinyang‘anyiro cha tuzo hiyo, ambayo hupigiwa kura na mwandishi Habari mmoja katika kila taifa kati ya 100 yanayoorodheshwa ya juu katika viwango vya FIFA.

Frankreich, Saint-Denis | Kylian Mbappe beobachtet UEFA-Qualifikationsspiel Frankreich gegen Griechenland
Mchezaji Kylian MbappePicha: Tnani Badreddine/DeFodi Images/picture alliance

Awali, mchezaji mwenza wa Messi katika timu ya taifa iliyoshinda Kombe la Dunia Emiliano Martinez alishinda tuzo ya Lev Yashin ya kipa bora ulimwenguni.

Kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa ya England Jude Bellingham alishinda Kombe la Kopa la mchezaji bora mwenye umri wa chini ya miaka 21. Mchezaji mwenzake wa Real Madrid Vinicius Jr. alitunukiwa Tuzo ya Socrates kwa kazi yake ya kibinaadamu nje ya uwanja.

Mshindi wa Kombe la Dunia la Wanawake wa Uhispania na kiungo wa Barcelona Aitana Bonmati alishinda Ballon d'Or kwa upande wa wanawake. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alitajwa kuwa mchezaji bora wa Kombe la Dunia. Aidha alitamba wakati Barcelona ikishinda Kombe la Mabingwa Ulaya msimu uliopita na hivi karibuni alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa UEFA.

 

(Reuters, Afp)