Ligi ya Uhispania yazitetea Real Madrid, Atletico Madrid
15 Januari 2016Baada ya Real Madrid na Atletico Madrid kuadhibiwa kwa madai ya kukiuka sheria za kuwasajili wachezaji watoto, ligi hiyo imeushutumu “utoshelevu wa sheria za ulinzi” wa wachezaji wa umri mdogo na ikasema “hazimlindi mtoto”.
Ligi hiyo inasema kandanda la Uhispania, kupitia vilabu vyao, inaunga sera ya kuwalinda watoto wenye umri mdogo na wasiwasi wa maendeleo yao na mafunzo wanayopewa.
Na baada ya mafanikio makubwa ya ushindi wa mabao tano kwa bila dhidi ya Derpotivo la Coruna kwenye mchuano wake wa kwanza kama kocha, Zinedine Zidane anatarajia mambo kuwa hivyo wakati Real Madrid itakapoikaribisha Sporting Gijon kesho Jumapili.
Barcelona wako mbele ya Real na pengo la pointi mbili na wana mchuano mmoja zaidi ya watani wao hao wa jadi, lakini wanakabiliwa na mtihani mkali kesho watakapowaalika Athletic Bilbao uwanjani Camp Nou.
Atleti ambao wanaonmgoza msimamo wa ligi kwa sasa pia walipigwa marufuku na FIFA kuwasajili wachezaji wapya kwa mwaka mmoja lakini wanatarajia kuyaweka hayo kando watakapopiga dhidi ya Las Palmas kesho.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Gakuba Daniel