1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya soka ya China, Njia panda kuendelea tena

Deo Kaji Makomba
19 Juni 2020

Wakati baadhi ya nchi duniani zikianza kulegeza taratibu vizuizi ilivyokuwa imeviweka ikiwemo kupigwa marufuku mikusanyiko na shughuli mbalimbali za kijamii kama vile michezo, huko nchini China hali bado si shwari

https://p.dw.com/p/3e2FV
Fußball ASIAN-Cup 2019 Thailand v China
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya China, Gao Lin akipiga shuti kufunga goli wakati wa michuano ya kombe la AFC Asian, wakati China ilipocheza na Thailand katika uwanja wa Hazza Bin Zayed huko Al-Ain mnamo Januari 20, 2019Picha: Getty Images/AFP/G. Cacace

Wakati baadhi ya nchi duniani zikianza kulegeza taratibu vizuizi ilivyokuwa imeviweka ikiwemo kupigwa marufuku mikusanyiko ya watu na shughuli mbalimbali za kijamii kama vile michezo, huko nchini China hali inaonekana bado si shwari baada ya kutokea maambukizi mapya katika mji wa Beijing.

Yaelezwa kuwa kutokea kwa mlipuko wa virusi vya corona mjini Beijing kumetatiza mikakati ya kuanza tena kwa ligi kuu ya soka nchini China, (CSL), mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya katika chama cha soka nchini China alisema.

Chama cha soka nchini China kilipanga kuanza ligi hiyo mnamo mwezi Februari mwaka huu, lakini kimeahirisha kuanza tena kwa ligi hiyo kwa muda usiojulikana kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19, unaosababishwa na virusi vya Corona.

Akizungumza katika runinga ya taifa, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza, Zhang Wenhong, alisema kuwa mlipuko wa virusi vya Corona mjini Beijing, ambako kumekuwa na visa vya maambukizi zaidi ya 180 vilivyorekodiwa kwa zaidi ya wiki moja sasa, kunaweza kusababisha kuchelewesha zaidi kuanza kwa kindumbwendumbwe cha ligi kuu ya soka ya China.

Ratiba ya mechi za soka China yaendelewa kujadiliwa

"Ratiba ya michuano ya ligi hiyo bado inajadiliwa kwa sababu janga hilo limelipuka tena mjini Beijing," alisema Zhang. "Ueneaji wa virusi vya Corona kutoka Beijing, kunaleta ugumu zaidi. Nadhani viongozi wa CSL wana wasiwasi juu ya hilo na wataendelea kubadilisha ratiba."

Aidha Zhang alibainisha kuwa ligi za mpira wa miguu barani Ulaya zilianza kurejesha misimu ya ligi zao baada ya kusimamishwa kwa muda kwa miezi kadhaa kwa sababu ya Covid 19 lakini alisema kuwa uongozi wa soka la China ulikuwa unachukua tahadhari zaidi.

"Nchi za Ulaya zimechukua uamuzi wa kuanza tena michezo yake ya ligi, kwa sababu wanaamini ikiwa wanaweza kudhibiti visa vya maambukizi ya virusi vya Corona na mfumo wa matibabu katika nchi hizo unafanya kazi vizuri, hivyo itakuwa sawa kuanza tena kwa michezo," alisema.

Coronavirus | China Peking Großmarkt von Yuegezhuang Desinfektion-Team
Wanachama wa kikundi uokoaji cha Blue Sky cha Beijing wakiendesha zoezi la kupulizia dawa katika soko la kuuza jumla huko Yuegezhuang Beijing.Picha: picture-alliance/Xinhua/Chen Zhonghao

"Hata hivyo lengo letu hapa China ni kuhakikisha tunadhibiti visa vya maambukizi ya virusi hivyo hadi kufikia kiwango cha chini kwa hivyo sisi ni wenye busara zaidi na bado tunahitaji muda zaidi."

Kwa upande wake Mkurugenzi wa utawala wa michezo wa Shanghai aliliambia Shirika la habari la taifa, Xinhua wiki hii kwamba ligi ya soka ya CSL itaanza tena mnamo mwezi Julai mwaka huu, ikiwa kila kitu kitaenda vyema.

Vizuizi vilivyowekwa kufuatia mlipuko wa virusi vya Corona, kumeleta athari kubwa katika soka la China na vilabu vya soka vikiathirika kutokana na matatizo ya kifedha, ikiwemo chama cha soka cha China, CSL," alisema Tianjin Tianhai.

Tangu kutokea kwa mlipuko wa virusi vya Corona, China imekuwa mwangalifu juu ya kurejesha tena mashindano ya michezo mbalimbali, licha ya majirani zake Koroea ya kusini, Japani pamoja na Taiwan zimeanzisha tena ligi za mpira wa miguu.

Nayo ligi kuu ya mpira wa kikapu nchini China itaanza tena Jumamosi tarehe (20.06.2020) katika viwanja viwili vya kati huko Qingdao na Dongguan lakini mashabiki hawataruhusiwa kuingia viwanjani.

 

Reuters