1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya mabingwa kutimua vumbi tena wiki hii

6 Novemba 2023

Kocha wa Dortmund amewaambia wachezaji wake wasahau kichapo cha Bayern katika pambano dhidi ya Newcastle.

https://p.dw.com/p/4YTFY
Newcastle United v Borussia Dortmund - UEFA Champions League - Group F
Dortmund baada ya mechi dhidi ya Newscastle Ligi kuu ya Mabingwa Ulaya.Picha: Carl Recine/REUTERS

Kocha wa Borussia Dortmund Edin Terzic anatumai timu yake haitozingatia kichapo cha 4-0  kutoka kwa Bayern Munich wakati watakapoikaribisha Newcastle United katika mechi ya Jumanne ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

"Tumekuwa wawazi kwa kila mmoja wetu. Tunataka kufanya vizuri zaidi haraka iwezekanavyo. Tunajua tunayo ndani yetu," aliwaambia wanahabari Terzic. Ushindi wa 1-0 walioupata Newcastle wiki mbili zilizopita unapaswa kuwatia moyo Dortmund. 

Kiungo Salih Özcan pia ana imani Dortmund itaonyesha majibu chanya.

Mabingwa watetezi Manchester City wanatarajia kukipiga na Young Boys katika uga wa nyumbani wa Etihad. PSG itasafiri kuelekea katika uga wa San siro kukipiga na AC Milan. Borussia Dortmund itakuwa nyumbani kuchuna na New Castle.  Lazio itacheza na Feryoon na Porto itaialika Antwerp.

Soma pia: Mabingwa watetezi wa ligi ya mabingwa Ulaya Manchester City yasafisha njia kuelekea hatua ya makundi

Baada ya miaka miwili ya masaibu katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, Barcelona wana nafasi ya kujikatia tiketi ya raundi ya mtoano dhidi ya Shakhtar Donetsk hapo kesho mjini Hamburg.

Mabingwa hao wa Uhispania wanaweza kujihakikishia kusonga mbele kwa ushindi wa nne mfululizo katika Kundi H, jambo ambalo hawajafanikiwa tangu 2021, walipobanduliwa na Paris Saint-Germain katika hatua ya 16 bora.

Bila shaka Barcelona wameimarika tangu Xavi alipowasili Novemba mwaka huo, na kutwaa ubingwa wa La Liga msimu uliopita, lakini bado wametatizika barani Ulaya.

Siku ya Jumatano, wawakilishi wengine wa Ujerumani RB Saalzburg itakuwa mwenyeji wa Inter Milan na Bayer Munich itacheza na Galatasaray.Union Berlin ambayo inaendelea kutoa matokeo duni msimu huu itakuwa ugenini katika uga wa Diego Armando Maradona. Arsenal inacheza na Sevilla na Real Madrid itacheza na Braga.