Ligi ya mabingwa barani Ulaya kundi F ni la kifo
30 Agosti 2019Mabingwa watetezi Liverpool wana miadi na SSC Napoli tena. Barcelona , Dortmund na Inter, wakiwa kwa jumla zimeshinda mara tisa vikombe vya Ulaya baina yao, wamewekwa pamoja katika kundi F pamoja na mabingwa wa Jamhuri ya Cheki Slavia Prague.
Baada ya kupokea kipigo dhidi ya Liverpool msimu uliopita, Lionel Messi na Barcelona wanaendelea kuwa timu inayopigiwa upatu kusonga mbele wakati wakiwania taji lao la kwanza la Champions League tangu mwaka 2015.
Dortmund ilishinda taji hilo mwaka 1997 na kushindwa katika fainali ya mwaka 2013. Ikiwa sasa inapata mafunzo kutoka kwa kocha Antonio Conte, Inter Milan iliishinda Barcelona katika nusu fainali kuelekea ushindi wa hivi karibuni kabisa wa mataji yake matatu mwaka 2010.
"Hili kwa kweli ni kundi gumu sana, ambalo linaifanya kuwa changamoto kubwa zaidi kwetu," amesema kocha wa Dortmund , Lucien Favre.
Liverpool ilisonga mbele katika kundi lake kwa gharama ya Napoli msimu uliopita na kufanikiwa kulinyakua taji hilo , likiwa taji lake la nne katika historia ya klabu hiyo mjini Madrid, na kikosi cha Carlo Ancelotti sasa kina fursa kwa mara nyingine tena ya kulipa kisasi.
Vilabu vyote hivyo vinatarajiwa kusonga mbele kutoka kundi E, ambalo linakamilishwa na mabingwa wa Austria Salzburg na Genk ya Ubelgiji.
Liverpool tena na Napoli
"Napoli tena," sifahamu sasa ni mara ya ngapi nakumbana na Napoli, lakini ni timu bila shaka yenye uzoefu mkubwa," amesema kocha wa Liverpool Juergen Klopp, ambaye amekumbana na Wataliani hao akiwa na Dortmund katika mwaka 2013-14 katika awamu ya makundi.
Liverpool inataraji kurejea katika fainali ya mwaka huu ambayo itafanyika Istanbul, ambako walishinda taji lao la tano mwaka 2005.
Baada ya kushindwa katika fainali ya msimu uliopita, Tottenham Hotspur inaweza kutarajia kukutana na mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich katika kundi B.
Huo utakuwa mpambano wao wa kwanza tangu mwaka 1983-84 katika kombe la UEFA. Watakutana pia na mabingwa wa Ugiriki Olympiakos pamoja na Red Star Belgrade ya Serbia, mabingwa wa mwaka 1991 wa kombe la Ulaya la washindi , katika kundi B.
Baada ya kushinda ligi ya Uropa , Chelsea wanarejea katika Champions League na wana miadi na timu iliyofikia nusu fainali msimu ulipita katika Champions League , Ajax pamoja na makamu bingwa wa champions League wa zamani Valencia pamoja na Lille ya Ufaransa katika kundi H.
Mabingwa wa Premier League Manchester City wamepewa kundi laini miongoni mwa timu zote wawakilishi wa England katika Champions League, ambapo vijana wa Pep Guardiola watapambana na Atalanta Bergamo ambao ndio kwanza wanaionja Champions League pamoja na Shakhtar Donestsk na Dinamo Zagreb katika kundi C.
City iliishinda Shakhtar mabao 3-0 nchini Ukraine katika awamu ya makundi msimu uliopita kabla ya kuikandika mabao 6-0 katika mchezo wao wa mwisho.
Real na PSG
Kutakuwa na mapambano mengine ya kupendeza kati ya wapinzani wanaofahamiana kwingineko, ambapo kikosi cha Zinedine Zidane cha Real Madrid kitarejesha mahusiano ya kufahamiana na Paris Saint-Germain katika kundi A. Real iliwaondoa mabingwa hao wa Ufaransa katika awamu ya timu 16 zilizobakia katika champions league katika njia yao kuelekea uibngwa wao misimu miwili iliyopita.
Mabingwa wa Uturuki Galatasaray na Club Brugge ya Ubelgiji wanakamilisha kundi A. Cristiano Ronaldo na Juventus Turin watakabiliana na Atletico Madrid tena baada ya kukiangusha kikosi hicho cha Uhispania katika awamu ya timu 16 msimu uliopita.
Pia watapambana na Bayer Leverkusen na Lokomotiv Moscow katika kundi D.
Pengine sehemu ambayo ina uwiano mzuri inazikutanisha Zenit saint Petersburg , Benfica , Lyon na RB Leipzig ambazo zitapambana katika kundi G. Michezo ya kwanza ya makundi yote itafanyika Septemba 17 na 18.