1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yapata Waziri Mkuu mpya

15 Oktoba 2012

Bunge la Libya limemchagua waziri mkuu mpya. Ali Zeidan, mwanadiplomasia wa zamani na mkosoaji mkubwa wa utawala wa rais aliyeondolewa madarakani Muamar Gaddafi, amesema suala la usalama ndilo atakalolipa kipaumbele.

https://p.dw.com/p/16Q1f
Waziri Mkuu mpya wa Libya Ali Zeidan
Waziri Mkuu mpya wa Libya Ali ZeidanPicha: Reuters

Ali Zeidan amechaguliwa katika kura iliyopigwa bungeni usiku wa kuamkia leo, akipata jumla ya kura 93 katika bunge lenye viti 200, akimshinda mpinzani wake, waziri wa serikali za mitaa Mohammed Al-Hrari ambaye alipata kura 85.

Kuchaguliwa huko kunamueka ana kwa ana na changamoto ya kuunda serikali inayokubaliwa na makundi yote ya kisiasa nchini Libya, na amepewa muda wa wiki mbili kuwa amelitimiza jukumu hilo.

Wakati serikali hiyo ikisubiriwa, Libya itaendelea kutawaliwa na ile ya mpito inayoongozwa na Abdulrahman al-Keib.

Mwanaharakati wa siku nyingi

Ali Zeidan ni mpinzani wa Gaddafi wa siku nyingi
Ali Zeidan ni mpinzani wa Gaddafi wa siku nyingiPicha: AP

Zeidan ambaye alikuwa mpinzani mkali wa rais aliyetimliwa madarakani Kanali Mouamar Gaddafi, alichaguliwa kuingia bungeni kama mgombea binafsi, lakini katika uchaguzi huu ameungwa mkono na na chama cha kiliberali, National Forces Alliance, NFA. Alilazimika kujiuzulu kiti chake bungeni ili kugombea wadhifa wa waziri mkuu.

Chama cha NFA kinavyo viti 39 kati ya 80 vilivyotengwa kwa ajili ya vyama vya kisiasa, na kiongozi wake Mahmud Jabril, alishirikiana na Zeidan kulifanya vuguvugu dhidi ya Gaddafi litambuliwe na jumuiya ya kimataifa.

Ali Zeidan anachukuwa nafasi iliyoachwa wazi na mtangulizi wake Mustafa Abushagur ambaye bunge lilipiga kura ya kutokuwa na imani naye takribani wiki moja iliyopita, baada ya serikali aliyoiteua kupingwa ndani ya bunge na nje yake.

Mustafa Abu Schagur, bunge lilipiga kura ya kutokuwa na imanai nae
Mustafa Abu Schagur, bunge lilipiga kura ya kutokuwa na imanai naePicha: picture-alliance/dpa

Libya inahitaji haraka serikali imara ili kuweza kuikarabati nchi iliyiharibiwa na vita, na vile vile kurejesha utengamanao miongoni mwa raia baada ya mafarakano yaliyosababishwa na mapigano yaliyomng'oa Gaddafi madarakani.

Usalama ndio kipaumbele

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuchaguliwa kwake, waziri mkuu huyu mpya amesema suala la usalama ndilo litakalopewa kipaumbele, kwa sababu ndilo mzizi wa matatizo yote yanayoikumba Libya kwa wakati huu. Amesema serikali yake itakuwa kama uongozi wa dharura utakaojaribu kutafuta suluhu kwa mgogoro uliopo.

''Uislamu ni dini yetu, na ni chimbuko la sheria zote. Chochote kinachokwenda kinyume na sheria za kidini, tunakikataa'' Alisema Zeidan.

Libyan protesters gather on the rubble of a destroyed section of the mausoleum of Al-Shaab Al-Dahman near the centre of Tripoli on August 26, 2012 to condemn attempts to demolish it and to protest against Islamic extremism. Islamist hardliners bulldozed part of the revered mausoleum in Tripoli in the second such attack in Libya in two days. AFP PHOTO/MAHMUD TURKIA (Photo credit should read MAHMUD TURKIA/AFP/GettyImages)
Picha: Mahmud Turkia/AFP/GettyImages

Wakati wa utawala wa Gaddafi, Libya haikoongozwa kwa misingi ya kidini, lakini kuangushwa kwake kumeyapa nguvu makundi yenye misimamo ya kiislamu, na pia yale ambayo hayapendelei masuala ya dini kuchanganywa na siasa. Imejitokeza pia migawanyiko kwa misingi ya kikabila na kimajimbo.

Bado njia ndefu

Zeidan atakabiliwa na changamoto kubwa inayotokana na kutapakaa kwa silaha, huku njia ya kuelekea kwenye maridhiano ikiwa bado ndefu, mwaka mmoja baada ya kuangushwa na kuuawa kwa kanali Muamar Gaddafi.

Ali Zeidan ni mwanasheria aliyejishughulisha na haki za binadamu. Aliwahi kuwa mwanadiplomasia wa Libya enzi ya rais Muamar Gaddafi, lakini alikosana na rais huyo na kuikimbia nchi mwaka 1980 akiwa balozi wa nchi yake nchini India. Baadaye alijiunga na chama cha ukombozi wa Libya ambacho kiliundwa na wanaharakati waliokuwa uhamishoni mwaka 1981, kabla ya kuhamia mjini Geneva ambako alijibiidisha na kutetea haki za binadamu nchini Libya.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpa/AFP/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef